Anayedaiwa kumuua mkewe kisha kumchoma moto awatolea uvivu waandishi wa habari mahakamani

Muktasari:

Upande wa mashtaka katika kesi inayomkabili Mfanyabiashara Hamis Said  Luongo (38) kwa kumuua mkewe kisha kumchoma moto kwa mkaa, Naomi Marijani umedai kuwa upelelezi bado haujakamilika huku mshatakiwa huyo akitoa onyo kwa waandishi wa habari wanaompiga picha.

Dar es Salaam. Hamis Said Luongo(38) ambaye ni mshtakiwa wa mauaji ya mke wake, Naomi Marijani katika eneo  la Gezaulole Kigamboni ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam nchini Tanzania kuwa atafanya kitu kibaya kwa waandishi wa habari ambacho mahakama hiyo haitakitarajia.

Awali, Wakili wa  Serikali Mwandamizi Wankyo Simon amedai leo Jumanne Agosti 13,2019 mbele ya Mahakama hiyo kuwa shauri lilikuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi haujakamilika.

Baada ya maelezo hayo, mshtakiwa Luongo alinyoosha kidole na kuiomba Mahakama hiyo kuwa kichwa chake kimechanganyikiwa hivyo atafanya kitu kibaya kwa waandishi wa habari ambapo Mahakama hiyo haitatarajia.

"Mheshimiwa nina kitu ambacho nataka nikueleze kuhusu waandishi wa habari ambao wamekuwa wakinipiga picha kuanzia chini hadi ndani ya mahakama, sasa nakueleza hivi nitakuja kuishangaza mahakama hii nitafanya kitu kibaya ambacho hamtakitegemea.”

"Kuna kesi ambayo inanikabili na sielewi hatima ya kesi yangu, hapa nilipo kichwa changu kimevurugika nina mawazo ya mtoto wangu na ninapofika hapa ndani nataka  akili yangu itulie lakini hawa wapiga picha wananipiga picha sasa nawaeleza kuwa nitawafanya kitu kibaya ambacho Mahakama haitatarajia," amedai

Baada ya kauli hiyo, Wakili Wankyo alimueleza mshtakiwa huyo kuwa kupigwa picha ni hali ya kawaida na washitakiwa wote wanaofikishwa mahakamani wanapigwa picha na yeye siyo mtu wa kwanza hivyo awape uhuru waandishi wa habari wafanye kazi yao kuwa huru.

"Lengo la waandishi wa habari ni kutoa habari na kuwajuza wananchi  hivyo awape uhuru  wafanye kazi yao kuwa huru na kumbuka hii ni mahakama na hatujui kitu unachotaka kufanya ni kitu gani," amedai Simon.

Baada ya kueleza hayo, Hakimu Ally ameahirisha kesi hiyo hadi Agosti 27, 2019 kwa ajili ya kutajwa.

Mshtakiwa huyo ameshitakiwa chini ya Kifungu  cha 196 cha Kanuni ya Adhabu, sura ya 16 kilichofanyiwa marejeo mwaka 2002.

Katika kosa hilo, mshitakiwa anadaiwa  Mei 15, 2019 katika eneo la Gezaulole Kigamboni Dar es Salaam  alimuua mtu anayeitwa Naomi Marajani.