VIDEO: Anayepumulia mashine achukuliwa na gari la wagonjwa kwenda Mloganzila

Muktasari:

Baada ya kutohudhuria kliniki kwa kipindi cha miezi mitatu, mgonjwa anayeishi kwa kupumulia mashine Hamad Awadh (28) leo amechukuliwa na gari ya wagonjwa kupelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili - Mloganzila kwa ajili ya kuonwa na jopo la madaktari kwa matibabu zaidi.

Dar es Salaam. Miezi mitatu baada ya kushindwa kuhudhuria kliniki, mgonjwa anayeishi kwa kupumua kwa mashine Hamad Awadh (28) amechukuliwa na gari la wagonjwa kuelekea Hospitali ya Taifa Muhimbili- Mloganzila.

Awadh amechukuliwa nyumbani kwake Kipawa mchana wa leo Alhamisi Septemba 12, 2019 na gari ya wagonjwa kutoka Mloganzila.

Mgonjwa huyo ambaye ameondoka nyumbani kwake saa 06:45 mchana, ameonyesha kupata matumaini baada kushindwa kwenda kliniki kutokana na kukosekana kwa usafiri rafiki.

Awali,  saa 3:30 leo asubuhi gari la wagonjwa kutoka Hospitali ya AgaKhan ilifika nyumbani kwa Awadh kwa ajili ya kutekeleza ahadi ya kutoa usafiri huo ili mgonjwa huyo akafanyiwe vipimo.

Hata hivyo dakika chache baadaye iliwasili gari la wagonjwa kutoka Mloganzila.

Awadh mwenyeji wa Mtama, Lindi akizungumza na Mwananchi Septemba 3 alisema tangu aliporuhusiwa kutoka hospitalini, alitakiwa kuhudhuria kliniki kila baada ya wiki mbili jambo ambalo hajalifanya mpaka sasa kutokana na mazingira magumu aliyonayo.

“Kiafya nazidi kuzorota, awali nilikuwa chini ya uangalizi wa madaktari lakini sasa najitegemea na sijapata huduma kwa muda mrefu. Siwezi kurudi kliniki sababu mashine siwezi kuichomoa kutoka hapa nikavumilia mpaka hospitali.”

Juni 10 mwaka huu, Hospitali ya Taaluma na Tiba – Mloganzila ilimpa msaada wa mashine hiyo ya kumsaidia kupumua yenye thamani ya Sh4 milioni, kutokana na matatizo yake ya afya ambayo yanamlazimu kutumia mashine ya oksijeni muda wote ili aweze kupumua.

Awadhi alifikishwa Hospitali ya Taifa Muhimbili- Mloganzila Julai 9 mwaka 2018 na kuruhusiwa Juni 9 mwaka 2019 baada ya afya yake kuimarika.