Asasi za kiraia zajipanga kuishtaki Serikali ya Tanzania

Muktasari:

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) wamesema wanatafakari kuIshtaki Serikali ya Tanzania katika kamisheni ya Umoja wa Afrika kwa kutaka kujitoa kwenye itifaki ya Mahakama ya Haki za Binadamu ya Afrika.

Dar es Salaam. Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) wamesema wanatafakari kuIshtaki Serikali ya Tanzania katika kamisheni ya Umoja wa Afrika kwa kutaka kujitoa kwenye itifaki ya Mahakama ya Haki za Binadamu ya Afrika.

Katika barua iliyosainiwa na Waziri wa Mambo ya Nje  wa Tanzania, Profesa Palamagamba Kabudi ya Novemba 21, 2019, inaeleza nia ya Tanzania kujiondoa kwenye mahakama hiyo ili kutafakari suala hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Desemba 4, 2019  jijini Dar es Salaam mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa amesema hatua ya kwanza ni kujadiliana na Serikali wakati wakiendelea kuangalia uwekezako wa kupinga hatua hiyo kwenye mahakama hiyo.

“Tutajaribu kupinga kwa sababu kwa sasa sheria na kanuni ziko kimya hazionyeshi utaratibu wa nchi inayojitoa watu wanaweza kwenda kwenye mahakama hiyohiyo kufungua kesi.”

“Ikishindikana hiyo tutakwenda kupitia kamisheni kule Banjul (Gambia) kwa sababu Tume ya Haki za Binadamu ya Afrika ndiyo mama wa hii mahakama,” amesema Olengurumwa.

Amesema mahakama hiyo iliundwa baada ya kuonekana tume ya haki za binadamu ya Afrika haikuwa na nafasi ya kusikiliza kesi.

Mkurugenzi wa LHRC, Anna Henga amesema kusudio la Serikali kujitoa katika mahakama hiyo litasababisha gharama kubwa kwa wananchi kupeleka kesi zao  Tume ya Haki za Binadamu ya Afrika nchini Gambia.

“Mtu atafute visa, atafute gharama za ndege, mwanasheria  wa kwenda kule lakini hapa Arusha unaweza kwenda hata kwa Bajaji. Kwa hiyo ile access to justice (uwezekano wa kupata haki) unakuwa mgumu mno,” amesema Henga.