Askari watawanywa maeneo ya Mlima Kilimanjaro

Muktasari:

Oktoba 11, 2020, mchana moto ulizuka katika eneo la Whona, ambako ni kituo cha kupumzikia wageni, wanaotumia njia ya Mandara na Horombo.

Moshi. Moto uliozuka katika Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro, Oktoba 11,2020, tayari umedhibitiwa na vikosi vya askari vimetawanywa katika maeneo ya mlima huo kwa ajili ya tahadhari.

Moto huo ambao umeteketeza kilomita za mraba 95.5,sawa na asilimia 5 ya eneo lote la hifadhi hiyo lenye kilomita za mraba 1,700, ulianzia Whona ambako ni kituo cha kupumzikia wageni wanaotumia njia ya Mandara na Horombo.

Akitoa taarifa leo oktoba 16, 2020, Kamishna Msaidizi Mwandamizi kitengo cha Mawasiliano, HIfadhi za Taifa (Tanapa)Pascal Shelutete, amesema  moto huo tayari umedhibitiwa hasa kwenye maeneo ya tambarare juu ya mlima.

Amesema licha ya udhibiti huo, bado vikosi vya askari vimetawanywa katika maeneo yote ya mlima kwa ajili ya tahadhari na kwamba udhibiti umetokana na kazi kubwa inayoendelea kufanyika tangu kutokea kwa moto huo Oktoba 11,2020, mchana.

Hata hivyo, shughuli za utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro, zinaendelea kama kawaida na hazijaathiriwa na moto huo.