Askofu Munga amkosoa Kardinali Pengo

Friday November 22 2019

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Moshi. Askofu Stephen Munga wa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), ameibua mjadala baada ya kuwakosoa waziwazi baadhi ya viongozi wa dini, akiwemo Polycarp Kardinali Pengo, kwa kauli walizotoa hivi karibuni.

Askofu Munga amesema viongozi hao wa kidini waliongea kupitiliza na kwamba mitazamo ya baadhi yao si ya viongozi wote wa kiimani.

Pengo na wengine walitoa kauli zinazopingwa na Askofu Munga wakati wa mkutano ulioitishwa hivi karibuni na mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwa ajili ya kuwaonyesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyo eneo lake la utawala.

Katika mkutano huo, viongozi hao walipitisha azimio la kumpongeza Rais John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri aliyoifanya ndani ya miaka minne.

Viongozi waliopata fursa na kumpongeza Rais katika mkutano huo ni Pengo, sheikh wa mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum na Askofu Alex Malasusa wa Dayosisi ya Mashariki ya KKKT.

Katika maoni yake, Pengo aliyekuwa askofu mkuu wa Jimbo Kuu la Katoliki la Dar es Salaam, alisema Makonda anafaa kumrithi Rais Magufuli baada ya kumaliza muda wake wa uongozi.

Advertisement

“Tunajiuliza baada ya Magufuli atakuwa nani ila mkiwepo wa aina yako (Makonda) wengi nisingekuwa na shaka ya kuwaza nani atafuata baada yake (Rais Magufuli),” alisema kiongozi huyo wa dini.

Naye Sheikh Mussa alisema katika kipindi cha miaka minne tu ya uongozi wa Rais Magufuli, amefanya mambo makubwa ya maendeleo ambayo hawakuyategemea.

Kiongozi wa Taasisi ya Wapo Mission International, Askofu Silvester Gamanywa, aliitaka CCM kumtunza Rais Magufuli akisema maendeleo yaliyofanyika ni miujiza.

Askofu Munga alivyowashukia

Lakini kauli hizo zinaonekana kutomfurahisha Askofu Munga na akaweka hisia zake katika mitandao ya kijamii, akisema walizungumza kupitiliza na akasema mitazamo yao si msimamo wa viongozi wote wa dini.

“Kwa maoni yangu wenzetu walizungumza kupitiliza (they overstated matters). Ni mitazamo yao na kamwe sio mitazamo ya viongozi wote wa kiimani,” anasema Askofu Munga katika andiko lake.

“Wenzangu viongozi wa kiimani katika mkutano ulioitishwa na Komredi Makonda na kupewa nafasi ya kuongea, kwa kweli mlijipendezesha. Sijui huko kwenu kiapo cha kichungaji kikoje,”alihoji askofu huyo.

Alisema kiapo chake kinamdai mchungaji aseme kweli hata kama amekaa mezani akila na Kaisari, kilichoandaliwa na Kaisari, lakini amwambie Kaisari mambo yake kwa ukweli.

“Ndugu zangu viongozi wa kiimani, akiwemo mtumishi niliyemheshimu sana, Muadhama Pengo, mmesema kwa kusifu kulikopitiliza mipaka (you overstated the matters you stated)”

“Tanzania ilikuwepo kabla ya Mheshimiwa Magufuli (Rais) na itakuwepo baada yake. Tanzania si mali ya mtu awaye yeyote bali ni mali ya Mungu muumbaji wa mbingu na nchi.”

Askofu Munga amesema Pengo alitoa kauli tata zinazoweka utukufu kwa wanadamu na si kwa Mungu.

Amesema anaweza kuwapuuza wengine waliozungumza, hakutegemea kama Pengo angetoa maneno ya aina hiyo.

“Mkumbuke Yesu Kristo aliyeungama maungamo mazuri mbele ya Pilato pasipo kuyumba. Huyu Kristo hakumpendezesha Pilato ili ahurumiwe na kupendelewa,” anasema katika andiko hilo.

“Mtasimamaje mbele zake Kristo siku ya hukumu? Kwa machozi baada ya kukusikiliza namwachia Bwana Yesu ahukumu juu yako. Mimi kamwe sitasema neno lolote la hukumu.

“Sina neno la kusema juu yako bali namwachia Kristo aliyekuita wewe na mimi katika utume huu. Wakati mwingine ni heri kunyamaza kuliko kusema na kupitiliza hata kukufuru.”

Askofu Munga alisema ataendelea kumheshimu Rais Magufuli na kwamba hana kibali cha kumhukumu, lakini akadai CCM inakandamiza vyama vya upinzani.

“CCM inakandamiza vyama vya upinzani na yeye kama mwenyekiti wa CCM arejee maamuzi ya CCM kuruhusu demokrasia ya vyama vingi vya siasa,” anasema.

“Akishafanya hivyo aangalie faulo zilizofanyika mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa. Aongee na Mungu aliyempa kibali kutawala nchi hii na kuona kama ametenda haki.”

Wadau wafunguka

Viongozi mbalimbali wa kisiasa waliohojiwa, walisema Askofu Munga ni miongoni mwa viongozi wachache wa kiroho wanaojitambua na wanaolitakia mema taifa.

Katibu wa Chama cha Kijamii (CCK), Renatus Muabhi alidai baadhi ya matamshi ya viongozi wa dini ya kuona kila kitu kiko sawa wakati taifa liko katika mkwamo yanasikitisha.

“Askofu Munga yuko sahihi. Baadhi ya viongozi wetu wa dini wanakosea sana. Kwa maneno aliyoongea Pengo napata shida hata ya kufika mbele yake.

“Kulikuwa na haja gani kwa Pengo kudai Makonda anafaa kumrithi Rais Magufuli?” alihoji Muabhi na kusema ndio maana anaungana na Munga kuwa kunyamaza nayo ni hekima.

Kwa upande wake, mkurugenzi mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga alisema Pengo na Munga wote wanatumia haki yao kutoa mawazo.

“Kama ni kweli lile andiko ni la Askofu Munga basi ametumia haki yake ya kikatiba ibara ya 19 kutoa maoni yake. Hakuna hata mmoja (Pengo na Munga) amevunja sheria,” alisema Henga.

Henga alisema hata mijadala inayoendelea katika mitandao ya kijamii kuhusu kauli ya Pengo na andiko la Askofu Munga, inapaswa kuendelea halafu jamii ipime ichukue lipi na lipi iache.

Kaimu katibu mwenezi wa chama cha UDP, Andrew Bomani alisema anaungana na Askofu Munga kwa asilimia 100 na akasema baadhi ya viongozi wa dini wanahitaji kuombewa.

“Nchi hii iko kwenye wakati mgumu sana. Unakuta baadhi ya viongozi wa dini wanaongea mambo mpaka tunaona wao ndio wanahitaji kuombewa sio kutuombea sisi,” alisema.

Hii si mara ya kwanza kwa Kardinali Pengo kuingia kwenye mzozo na viongozi wenzake wa kidini baada ya mwaka 2015 kuupinga waraka wa Jukwaa la Wakristo uliowataka wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kupiga kura na kushiriki kutoa elimu inayotakiwa na baadaye kupiga kura ya kuiokataa Katiba Inayopendekezwa.

Advertisement