Aslay bado hajafuta wazo la kolabo na Diamond

Thursday September 5 2019

 

By Rhobi Chacha, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Licha ya kuachia wimbo na Ali Kiba saa 24 zilizopita, msanii wa muziki nchini Tanzania,  Isihaka Nassoro maarufu Aslay amesema kiu ya kufanya kolabo na msanii mwenzake nchini humo Diamond ipo pale pale.

Akizungumza na MCL Digital leo Alhamisi Septemba 5, 2019 Aslay amesema kipindi cha nyuma kulikuwa na mipango ya kufanya remix ya wimbo wake 'Natamba' ili amshirikishe Diamond hata hivyo mambo hayakwenda vyema.

Amefafanua kila mmoja kwa upande wake katika mahojiano yake na vyombo vya habari alisema anatamani kufanya kazi na mwenzake.

 “Licha ya kushindikana hiyo Remix, ila muziki mzuri bado upo na wazo bado lipo kichwani hivyo ipo siku nitafanya naye wimbo wa pamoja" amesema Aslay.

Kuhusu kolabo yake na Ali Kiba ambaye ni msanii wa muziki nchini Tanzania amesema siyo tu mashabiki wake walitaka afanye bali  hata yeye alikuwa akitamani.

"Unajua kila mwanamuziki anaamini akifanya kazi na mwanamuziki fulani anajiachia na lazima mashabiki wafurahie.”

Advertisement

“Basi kwa upande wangu nilikuwa nikitamani siku moja kufanya kazi na Ali Kiba na hili naona limetimia na (wimbo) Bembea iko kitaani," amesema Aslay.

Amesema ndoto yake ilikuwa ni kufanya kolabo  na Kiba kwa sababu wanaendana hivyo itamrahisishia na atakuwa huru.

Wimbo huo wa Bembea ulioachiwa jana Jumatano, hadi kufikia leo Alhamisi saa 11.35 jioni ulikuwa umetizamwa You tube na watu 557,537.

Advertisement