Bendi ya TOT yapewa vyombo vipya

Muktasari:

Wanamuziki wa bendi  ya Tanzania One Theatre (TOT) wametakiwa kuwa wabunifu na kufanya kazi zaidi ya iliyokuwa ikifanywa na muasisi wa bendi hiyo,  Kapteni John Komba.

Dar es Salaam. Wanamuziki wa bendi  ya Tanzania One Theatre (TOT) wametakiwa kuwa wabunifu na kufanya kazi zaidi ya iliyokuwa ikifanywa na muasisi wa bendi hiyo,  Kapteni John Komba.

Hayo yameelezwa leo Ijumaa Novemba Mosi, 2019 na katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally alipokuwa akiikabidhi bendi hiyo vyombo vipya vya muziki vilivyonunuliwa na chama hicho tawala nchini Tanzania.

Amewataka wanamuziki  hao kuongeza ubunifu ili waendelee kuwepo kwenye soko la muziki wa dansi, kwamba kinyume na hapo wataendelea kubaki nyuma.

“Mnatakiwa kuwa wabunifu,  kila siku nawasikia wimbo mmoja tu, msipokuwa wabunifu akina Harmonize watawaacha mbali. Fanyeni kazi zaidi ya alivyokuwa Komba, nyimbo zake zimeacha alama.”

“Semeni mnataka nini, vifaa tumewapa kama kuna kingine mnahitaji niambieni mwenyekiti (Rais John Magufuli) amenielekeza niwasimamie kwa ukaribu,” amesema Dk Bashiru.

Dk Bashiru pia amewataka watunge nyimbo za kutosha kwa ajili ya hamasa kwa wanachama bila kusahau kutumia sanaa yao kuelimisha kuhusu changamoto zilizopo kwenye jamii.

 “ Kuna mambo mengi, mabadiliko ya tabia nchi yanavyoathiri mazingira, ni sehemu mnayotakiwa kufanyia kazi mkaelimishe jamii kupitia sanaa, bado masuala ya rushwa ni tatizo kote huko kunahitaji sanaa fanyeni kazi,”  amesisitiza.