Bosi shule za Zam Zam akutwa ofisini kwake amefariki dunia

Sheikh wa Mkoa wa Dodoma, Mustapha Rajabu

Muktasari:

Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma nchini Tanzania linaendelea na uchunguzi wa kifo cha Mkurugenzi wa Shule za Zam Zam za Dodoma aliyekutwa amefariki dunia ofisini kwake.

Dodoma. Mkurugenzi wa Shule za Zam Zam jijini Dodoma nchini Tanzania, Sheikh Rashid Bura amekutwa amefariki dunia ofisini kwake eneo la Majani ya Chai karibu na Nyerere square jijini humo.

Bura aliondoka nyumbani kwake zaidi ya siku nne zilizopita na hakujulikani alipokwenda ambapo juhudi za kumtafuta zilifanyika bila mafanikio hadi jana Jumatano Desemba 25, 2019 alipokutwa ofisi kwake akiwa amekufa huku mlango wa ofisi ukiwa umefungwa.

Sheikh wa Mkoa wa Dodoma, Mustapha Rajabu alikiri kuwapo kwa kifo hicho lakini akasema wasemaji ni Jeshi la Polisi huku akisema katika imani ya dini ya Kiislamu kifo kinaweza kumkuta mwanadamu mahali popote.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto hakuwa tayari kuzungumzia tukio hilo lakini alikuwapo wakati mwili huo unachukuliwa jana Jumatano saa moja jioni ukapelekwa mochwari ya Hospitali ya Rufaa ya Dodoma.

Msiba uko nyumbani kwake Mtaa wa Chang’ombe jijini Dodoma.