Bunge Tanzania laanza kufanya vikao katika kumbi mbili tofauti

Muktasari:

Kikao cha Bunge la Tanzania kwa mara ya kwanza  leo Aprili 15, 2020 kimefanyika huku wabunge wakiwa katika kumbi mbili tofauti.

Dodoma. Kikao cha Bunge la Tanzania kwa mara ya kwanza  leo Aprili 15, 2020 kimefanyika huku wabunge wakiwa katika kumbi mbili tofauti.

Akizungumzia suala hilo Spika Job Ndugai amesema wanajaribu mitambo kwa kuwa teknolojia zipo za kutosha.

Katika kikao cha leo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Kapteni mstaafu George Mkuchika aliwasilisha hotuba ya makadirio ya mapendekezo ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2020/21 akiwa ukumbi mkuu wa Bunge.

Baada ya kumaliza Ndugai alimuita mwenyekiti wa kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za mitaa, Jason Rweikiza aliyekuwa ukumbi mwingine wa Msekwa ili asome maoni ya kamati hiyo.

Utaratibu huo ulipaswa kuanza kutumika kuanzia Machi 31, 2020 ulipoanza mkutano wa Bunge lakini suala hilo lilikuwa likiwekwa sawa na leo ndio umeanza rasmi.

Lengo la utaratibu huo ni  kupunguza wingi wa wabunge katika ukumbi mmoja ili kujikinga na maambukizi ya homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona.

 “Waheshimiwa wabunge  baada ya Waziri kumaliza kusoma hotuba yake, sasa naomba tutesti mitambo yetu namuita Mwenyekiti wa kamati mheshimiwa Jason Rweikiza na leo atasoma hotuba yake akiwa ukumbi wa Pius Msekwa naomba tumsikilize,” amesema Ndugai.

Wakati Rweikiza akisoma maoni yake, wataalamu wa picha waliweka picha mbili za kumbi hizo lakini mbunge huyo alionekana kama yupo ndani ya ukumbi mkuu kwani baadhi ya wabunge walikuwa kwenye ukumbi huo wakiendelea kufuatilia na wale wa ukumbi mkubwa walikuwa wakimfuatilia pia.