Bunge kuanza kesho, mrithi wa Tundu Lissu kuapishwa

Muktasari:

Vikao vya mkutano wa 16 wa Bunge la Tanzania vinaanza kesho Jumanne huku miswada mitatu ikitarajiwa kujadiliwa katika hatua ya pili na ya tatu pamoja na kushuhudia kiapo cha uaminifu.


Dodoma. Mkutano wa 16 wa Bunge la Tanzania utaanza kesho Jumanne Septemba 3, 2019 jijini Dodoma ambapo pamoja na mambo mengine itashuhudia Miraji Mtaturu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) akiapishwa kuwa mbunge wa Singida Mashariki.

Mtaturu anaapishwa kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Tundu Lissu wa Chadema ambaye Juni 28, 2019 Spika wa Bunge hilo, Job Ndugai alilitangazia Bunge kwamba amepoteza sifa za kuwa mwakilishi wa Singida Mashariki.

Spika Ndugai alitoa sababu mbili zilizomfanya Lissu kupoteza ubunge ni kutokujaza fomu za mali na madeni za viongozi wa umma pamoja na kutokutoa taarifa kwake (spika) ya wapi alipo.

Wakati Spika Ndugai alitoa taarifa hiyo, Lissu alikuwa nchini Ubelgiji akiendelea na matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 mchana wa Septemba 7, 2019 akitoka bungeni.

Ratiba iliyotolewa na Bunge la Tanzania mbali na kuelezea shughuli zitakazofanywa na mkutano huo wa 16 ni pamoja na kiapo cha uaminifu kwa Mtaturu ambaye alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida.

Katika harakati za kumrithi Lissu, Mtaturu alitangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa ubunge Julai 2019 baada ya washindani wake kutokurejesha fomu za kuomba kuteuliwa.

Hata hivyo, Lissu ambaye alikuwa Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni amefungua kesi Mahakama Kuu ya Tanzania kupinga kuvuliwa ubunge kesi ambayo inaendelea leo Jumatatu mahakamani hapo.

Katika ratiba ya Bunge, inaonyesha miswada hiyo ni wa Sheria ya Serikali Mtandao wa Mwaka 2019, Marekebisho ya sheria mbalimbali namba 4 na namba 5.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Bunge, kesho Bunge litaanza na kiapo cha uaminifu na baadaye maswali na majibu.

Ratiba hiyo ndogo ambayo inaonyesha kuwa pia kesho kutakuwa na  azimio la kumpongeza Rais John Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kuendesha mkutano wa 9 wa jumuiya hiyo.