Bunge la Tanzania lasifia uamuzi Serikali kujenga hospitali rufaa Chato

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii nchini Tanzania, Peter Serukamba

Muktasari:

Bunge la Tanzania kupitia Kamati yake ya Huduma ya Jamii limesifia  uamuzi wa ujenzi wa hospitali ya rufaa ya kanda wilayani Chato Mkoa wa Geita ambapo imesema litasaidia kwa wakazi wa maeneo hayo.

Dodoma. Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii nchini Tanzania, Peter Serukamba amesifia uamuzi wa Serikali kujenga Hospitali ya Rufaa ya Kanda wilayani Chato Mkoa wa Geita kuwa  utapunguza idadi ya wagonjwa wanaokwenda Hospitali ya Rufaa ya Bugando mkoani Mwanza.

Serukamba ameyasema hayo leo Jumatatu, Januari 20 2020 wakati Waziri ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alipowasilisha taarifa yao ya utekelezaji wa shughuli zake.

“Tuangalie Chato iko wapi? Fikirieni watu wa Kibondo, Kakongo, Kasulu, Ngara, Karagwe wote walikuwa wanakwenda Bugando. Kwa hiyo unakuta  Bugando imejaa. Tukipata another (nyingine) hospitali kama Bugando itasaidia. Kwangu mimi I don’t care (mimi sijali  imejengwa wapi?. Muhimu imejengwa katikati kwa hiyo itaokoa maisha ya watu wetu,” amesema.

Amesema kuhangaika na imejengwa wapi ni kupoteza mwelekeo na kwamba muhimu inajengwa eneo ambalo ni katikati na hivyo kuokoa maisha ya watu.

Awali,  Waziri Ummy aliiambia kamati hiyo kuwa Serikali inajenga Hospitali ya Rufaa ya Kanda katika wilaya hiyo.

Amesema sababu ya kujenga ni kuwa mikoa ya kanda ya ziwa kuwa na watu zaidi ya milioni 15.