CCM yatangaza mgombea jimboni kwa Nasari

Monday April 15 2019

 

By Elizabeth Edward, Mwananchi

Dar es Salaam. Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi, imempitisha Dk John Pallangyo kupeperusha bendera ya chama hicho kwenye uchaguzi wa ubunge, Arumeru Mashariki.

Kikao hicho kilichofanyika jijini Dodoma leo Jumatatu Aprili 15, 2019 kiliongozwa na mwenyekiti wa chama hicho, Rais John Magufuli pamoja na mambo mengine kilipitisha jina hilo na wagombea ujumbe wa kamati kuu ya CCM kupitia UVCCM kundi la bara.

Majina yaliyopitishwa kwenye ujumbe ni Sara Sompo, Ngusa Juda na Japhary Mghamba.

CCM imefanya uteuzi huo baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutangaza uchaguzi mdogo katika jimbo hilo ukitarajiwa kufanyika Mei 19, 2019.

Jimbo hilo lililokuwa likiwakilishwa na Joshua Nassari kwa tiketi ya Chadema lilitangazwa kuwa wazi baada ya mbunge huyo kupoteza sifa kufuatia kutohudhuria vikao vya mikutano mitatu ya Bunge mfululizo bila taarifa.

Machi 14, 2019 Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai aliandikia barua kwenda NEC akiarifu kuwa jimbo la Arumeru Mashariki lipo wazi kutokana na mbunge wa jimbo hilo kutohudhuria vikao vya mikutano mitatu mfululizo.

Advertisement

Advertisement