CWT yakerwa walimu kutokuwa waaminifu kusimamia mitihani

Tuesday September 10 2019Katibu Mkuu wa CWT, Mwalimu Deus Seif

Katibu Mkuu wa CWT, Mwalimu Deus Seif 

By Nazael Mkiramweni, Mwananchi. [email protected]

Dodoma. Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kimewataka waalimu nchini humo kurudisha uaminifu uliokuwepo awali katika suala la usimamizi wa mitihani na wasipofanya hivyo ipo siku vifaru vitahusika kulinda uaminifu wa waalimu wakati wa utekelezaji wa jukumu hilo.

Katibu Mkuu wa CWT, Mwalimu Deus Seif amesema hayo jijini Dodoma leo Jumanne Septemba 10, 2019 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mitihani ya darasa la saba itakayofanyika kesho Jumatano na keshokutwa Alhamisi.

Mwalimu Seif amesema uvujaji wa mitihani hautakiwi kuendelea na walimu wanapaswa kutambua kazi ya kufundisha iliisha wiki iliyopita hivyo wawaache wanafunzi wafanye mitihani yao.

“Natamani uaminifu uliokuwepo mwanzo urudi tena na waalimu wanajua zamani mitihani tulikuwa tunasimamia sisi hatukuwa na mgambo wala askari lakini kutokana na uaminifu kupungua tumepewa migambo walinde uaminifu wetu, wakaona haitoshi tukapewa jeshi la polisi na SMG kulinda uaminifu wetu,” amesema Mwalimu Seif

“Uaminifu huu ukizidi kupungua kuna siku tutapewa vifaru vije vilinde hiyo uaminifu wetu kwenye usimamizi wa mitihani, kwa hiyo niwaombe waalimu kuonyesha uaminifu mkubwa ili kulinda hadhi yetu ya ualimu.”

Hata hivyo, amewatakia heri wanafunzi wote wanaofanya mitihani ya kuhitimu darasa la saba pamoja na waalimu wanaohusika kusimamia mitihani hiyo kufanya kazi hiyo kwa uaminifu.

Advertisement

 

 

Advertisement