Chadema wasema hawana ushahidi Mchungaji Msigwa kulipiwa faini

Mkurugenzi wa Itikadi, uhusiano na mambo ya nje wa Chadema, John Mrema

Muktasari:

Baada ya Rais John Magufuli kumlipia Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa faini ya Sh38 milioni kati ya Sh40 milioni anazotakiwa kulipa, chama hicho kimesema tayari kimeshamlipia faini mbunge huyo wa Iringa Mjini.

Dar es Salaam. Baada ya Rais John Magufuli kumlipia Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa faini ya Sh38 milioni kati ya Sh40 milioni anazotakiwa kulipa, chama hicho kimesema tayari kimeshamlipia faini mbunge huyo wa Iringa Mjini.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Machi 12, 2020 Mkurugenzi wa Itikadi, uhusiano na mambo ya nje wa Chadema, John Mrema amesema, “sisi kama chama tumelipa Sh100 milioni ya watu watatu ambao ni Peter Msigwa, John Mnyika na Salum Mwalimu na tumewalipia kupitia benki tawi la Azikiwe.

“Tumeshapeleka malipo mahakamani, tunasubiri risiti za mahakama. Kama kuna mwingine amemlipia Mchungaji  Msigwa hatuna ushahidi na uhakika nao, kama chama mahakama haijaturejeshea fedha za Msigwa kwamba kalipiwa mara mbili.”

Mchungaji Msigwa amelipiwa faini hiyo na Magufuli huku maelezo ya malipo yakiwasilishwa leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa aliyeambatana na Mchungaji Beneth Msigwa aliyesema  kuwa ni ndugu wa Rais Magufuli.

“Baada ya hukumu familia (ya Mchungaji Msigwa) walitafuta Sh2 milioni na kwenda kwa Rais Magufuli ambaye aliongeza Sh38 milioni wakaenda kulipa. Hapa wameleta risiti na wanaelekea gerezani kwa ajili ya kumtoa Mchungaji Msigwa,” amesema Gerson Msigwa.

Mbunge huyo wa Iringa Mjini  ni kati ya viongozi wanane wa Chadema ambao pamoja na aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Vicent Mashinji Jumanne Machi 10, 2020 walihukumiwa kulipa faini ya Sh350 milioni au kwenda jela miezi mitano baada ya kutiwa hatiani kwa makosa 12 kati ya 13 yaliyokuwa yanawakabili.

Washtakiwa hao wakiongozwa na mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe walilazimika kwenda jela baada ya kushindwa kukamilisha taratibu za kulipa faini hiyo waliyohukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Baada ya hukumu hiyo iliyosomwa  na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, Chadema walianza kuchangishana fedha kwa ajili ya kuwalipia faini viongozi wake hao.

Hadi leo saa 9 alasiri, wabunge waliolipiwa faini na kutoka jela ni ni Ester Bulaya (Bunda), Esther Matiko (Tarime Mjini) na Halima Mdee (Kawe).

Ambao bado wapo katika gereza la Segerea ni Mbowe, John Heche (Tarime Vijijini),  John Mnyika (Kibamba), naibu katibu mkuu wa chama hicho-Zanzibar, Salum Mwalimu na Mchungaji Msigwa.