Hoja sita za Chadema kwa msajili

Wednesday October 9 2019

 

By Elias Msuya, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Chadema imekuja na hoja sita kumjibu msajili wa vyama vya siasa aliyewataka wajieleze kwanini wasichukuliwe hatua kwa madai ya kukiuka Sheria ya Vyama vya Siasa kwa kuchelewa kufanya uchaguzi mkuu wa chama hicho.

Barua ya Msajili ya Oktoba Mosi, 2019 iliyosainiwa na Sisty Nyahonza kwa niaba ya msajili, ilieleza kuwa uongozi wa Chadema chini ya mwenyekiti wake, Freeman Mbowe umemaliza muda wake tangu Septemba 14.

Msajili alikitaka chama hicho kutoa maelezo hayo kabla ya Oktoba 7, saa 9:30 alasiri.

Katika barua yao ya Oktoba 5, waliyomjibu Msajili, Chadema wamelitaja Jeshi la Polisi kuwa moja ya sababu za wao kuchelewa kufanya uchaguzi huo.

“Mara zote ambazo uchaguzi wa ndani ulikuwa ufanyike, chama kilipata vikwazo kwa kuzuiliwa na Jeshi la Polisi na kulazimika kusimama na kuahirishwa.

“Ofisi yangu ilikujulisha ili ofisi yako iingilie kati, kwa sababu vikao vya uchaguzi ni vya ndani na kwa hiyo havina haja ya kuomba kibali cha Jeshi la Polisi,” imesema moja ya aya ya barua hiyo iliyosainiwa na katibu mkuu wa chama hicho, Dk Vincent Mashinji.

Advertisement

Mashinji amefafanua kuwa tangu Julai hadi Oktoba mwaka huu, idadi ya majimbo na wilaya zilizokamilisha uchaguzi zimeongezeka na tayari wameanza chaguzi za mikoa wanazotarajia zikamilike Desemba ambayo ni muda ulioelekezwa na Kamati Kuu. “Ni vema pia kukujulisha kwamba pamoja na kuendelea kufanyika kwa uchaguzi wa ndani, bado katika baadhi ya maeneo Jeshi la Polisi limeendelea kuingilia uchaguzi wetu.”

Mashinji katika majibu hayo ameitaja barua waliyomwandikia Mkuu wa Jeshi la Polisi Septemba 30 wakilalamikia kuingiliwa kwenye chaguzi hizo.

Kuhusu kukata rufaa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani kwa mujibu wa kifungu cha 46(6) cha Sheria ya Jeshi la Polisi, Chadema wametaja kifungu cha 43(1) cha sheria hiyo, wakisema kinahusu mtu anayetaka kufanya maandamano na mikutano ya hadhara kutoa taarifa kwa ofisa mwandamizi wa Polisi (OCD), akikataliwa ndipo atakata rufaa.

“Hivyo vikao vya uchaguzi wa ndani, havihitaji kuomba kibali cha Polisi na kwa kurejea kifungu hicho umejielekeza vibaya,” imefafanua barua hiyo

Kuhusu madai ya Msajili kuwa hawajawahi kueleza na kuambatanisha ushahidi juu ya sababu za kusogeza mbele uchaguzi huo, chama hicho kimeeleza kuwa kilishawasilisha barua hizo.

“Tulishawasilisha kwako barua kadhaa tangu mwaka 2018 tukikujulisha juu ya zoezi la mafunzo na uchaguzi wa ndani wa chama na malalamiko juu ya Jeshi la Polisi kuingilia chaguzi za kata, majimbo, mikoa na kanda za chama,” imesema barua hiyo.

“Hata hivyo, nakukumbusha kwamba hukuwa unachukua hatua, inashangaza wakati huu ofisi yako kusema kwamba haina taarifa wala haijawahi kusikia,” imeongeza barua hiyo.

Kuhusu madai kuwa Chadema ilisema katika barua yake kuwa uongozi umemaliza muda, wamekanusha hilo na kudai kuwa walimpa taarifa Msajili kuhusu kuongezewa muda na kamati kuu.

Barua hiyo imefafanua kuwa uamuzi wa kusogeza mbele uchaguzi ngazi za Taifa na ngazi za chini, ulifanywa na mamlaka ya chama yenye nguvu ya katiba ya chama

Chadema imeinukuu barua ya Msajili ya Oktoba 2018 kwa makatibu wakuu wa vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu iliyoeleza suala la kuongeza muda wa uongozi wa chama.

“Ni lazima kuwe na sababu ya msingi, iwe inaruhusiwa na Katiba ya chama husika, kuwe na ukomo, kufanywe kwa mujibu wa Katiba na kanuni za chama na Msajili apewe taarifa.”

Kuhusu uhai wa uongozi kuwa miaka mitano, barua hiyo imetaja ibara ya 6.3.3 ya Katiba ya chama inayozungumzia kusogeza mbele uchaguzi wa ndani wa chama.

Chadema pia imesema barua ya Msajili haikuzingatia sababu zilizotolewa kwenye barua yao nyingine ya Septemba 11, 2019. “Ilieleza kusogeza mbele tarehe ya mkutano mkuu ili mkutano huo pia ufanye marekebisho ya Katiba iendane na mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya siasa.”

Chadema pia wameambatanisha vielelezo mbalimbali.

Advertisement