DC Sabaya amkabidhi kapteni mstaafu Takukuru

Tuesday December 3 2019

Tanesco Wilaya ya Hai, Theodory Hall, Fiber Board ,Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro nchini Tanzania, Lengai Ole Sabaya,

 

By Florah Temba, Mwananchi [email protected]

Hai. Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro nchini Tanzania, Lengai Ole Sabaya ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wilayani humo kumkamata na kumchunguza mkurugenzi wa Bodi ya Nyuzi, Kapteni mstaafu John Mushi.

Mushi anatuhumiwa kutumia vibaya mamlaka yake na kujimilikisha eneo la Serikali kinyume cha taratibu.

Eneo hio lenye ukubwa wa mita za mraba 3,371 mali ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) linadaiwa kumilikiwa na Mushi tangu mwaka 1984 huku kodi ikilipwa na Tanesco. Anadaiwa hana nyaraka zozote zinazomruhusu kufanya hivyo.

Sabaya pia ameagiza mali zilizokuwepo katika eneo hilo vikiwamo vifaa vya ujenzi kuzuiwa na mashine ya kufyatua matofali kupelekwa katika eneo la ofisi yake mpaka  Mushi atakapolipa kodi ya miaka 35 aliyolipiwa na Tanesco

Sabaya ametoa agizo hilo jana Jumatatu Desemba 2, 2019 baada ya kutembelea eneo hilo, kutoa siku 30 kwa Tanesco kuhakikisha wanazungusha ukuta eneo lote na siku 60 kuanza ujenzi wa jengo la kisasa.

Amesema Mushi alitambua eneo hilo ni mali ya umma lakini kwa makusudi amelihodhi kinyume cha taratibu na hata alipofuatwa na Tanesco awape eneo lao aliwatishia.

Advertisement

 “Takukuru nawakabidhi mtu huyu, fedha ya Serikali ambayo unajua imepotea kutokana na kulikalia eneo hili kinyume cha taratibu naitaka na kuanzia sasa Tanesco naomba muondoe mali zote hapa, vyote vitakaa eneo la halmashauri mpaka tutakapopata fedha za Serikali.”

 

“Huyu alikuwa mkurugenzi wa Fiber Board wakati ikiwa chini ya Serikali na eneo hili lilikuwa mali ya umma hivyo akiwa mkurugenzi wa taasisi hiyo ya Serikali wakawa wananunua magogo kuyaweka hapa,” amesema Sabaya.

 

Meneja wa Tanesco Wilaya ya Hai, Theodory Hall amesema eneo hilo lina ukubwa wa mita za mraba 7,271 na wamekuwa wakililipia kwa miaka yote mpaka walipotaka kuhakiki ndipo walipogundua sehemu ya eneo lao imevamiwa na mtu mwingine.

 

Akizungumzia eneo hilo Mushi amesema mbali na kukiri kuwa hakulinunua popote eneo hilo na wala hakuwahi kulilipia kodi, kwamba alipewa na halmashauri ya Hai mwaka  1982 baada ya kuandika barua.

 

Pamoja na maelezo yake hayo, ofisa ardhi wa Halmashauri hiyo, Jacob Muhumba amedai kiwanja hicho kilipangwa kwa matumizi ya umma, ni mali ya Tanesco akisisitiza kuwa hakuna nyaraka wala kumbukumbu yoyote inayomtaja mmiliki mwingine katika eneo hilo.

 

 

 

 

 

 


Advertisement