Daktari ‘aliyemuuza’ Osama akata rufaa

Islamabad. Daktari wa Pakistan, Shakil Afridi aliyeisaidia Marekani kumuua kiongozi wa kundi la al-Qaeda, Osama Bin Kaden amekata rufaa dhidi ya hukumu yake jela.

Jaji aliahirisha kesi hiyo ambayo kwa mara ya kwanza imesikilizwa katika mahakama ya wazi hadi Oktoba 22 kufuatia ombi la waendesha mashtaka.

Dk Afridi anadai alinyimwa haki yake wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo katika hatua ya awali, inaripoti BBC.

Ingawa hakushtakiwa kwa jukumu lake katika operesheni ya 2011 ya kumsaka na kumuua mtu aliyekuwa akitafutwa sana duniani, kufungwa kwake jela kulisababisha hisia tofauti hadi Marekani ikafuta mbali msaada wa dola 33 milioni kwa Pakistan.

Rais wa Marekani Donald Trump aliahidi katika uchaguzi wa 2016 kwamba atamwachilia huru Afridi baada ya dakika mbili iwapo atachaguliwa lakini hilo halijafanyika.

Huku daktari huyo akionekana kuwa shujaa Marekani, nchini Pakistan anaonekana kama msaliti ambaye anadaiwa alileta aibu kwa taifa hilo.

Na hatua hiyo ilizua maswali mengi ya iwapo Jeshi la Pakistan lilikuwa linajua iwapo Bin Laden alikuwa nchini humo.

Pakistan imesalia kuwa mshirika asiyeaminika katika vita vya Marekani dhidi ya wapiganaji wa Kiislamu.

Dk Afridi alikuwa daktari mkuu katika hospitali ya wilaya ya Khyber na akiwa mkuu wa huduma za afya alikuwa amesimamia baadhi ya mipango kadhaa ya chanjo zinazofadhiliwa na Marekani.

Kama mfanyakazi wa serikali, alianzisha mpango wa chanjo ya Hepatitis B, ikiwamo katika mji wa Abbottabad ili kubaini iwapo waliokuwa wakiishi katika eneo hilo ni nduguze bin Laden.

Inadhaniwa kwamba mfanyakazi mmoja wa Dk Afridi alitembelea nyumba ya akina Osama bin Laden na kuchukua vipimo vya damu  lakini haijulikani iwapo hilo lilisaidia Marekani kumpata Osama.

Dk Afridi alikamatwa Mei 23, 2011 siku chache tu baada ya Bin Laden kuuawa.

Familia yake imekuwa ikiishi katika maficho tangu kukamatwa kwake ikihofia shambulio la kijeshi.

Mkewe ni msomi kutoka Abbotabad ambaye alikuwa mwalimu mkuu wa Shule ya serikali kabla ya kwenda mafichoni. Wawili hao wana watoto watatu - wavulana wawili na msichana mmoja.

Mwezi Januari 2012 , maofisa wa Marekani walikiri hadharani kwamba Dk Afridi alikuwa akikifanyia kazi kikosi cha ujususi cha Marekani,  CIA, lakini haijulikani jukumu lake lilikuwa ni lipi.

Hata Dk Afridi hakujua ni nani aliyekuwa akilengwa katika operesheni hiyo, wakati alipoajiriwa na CIA kulingana na uchunguzi wa Pakistan.

Awali alikuwa ameshtakiwa kwa kutekeleza uhaini na alifungwa Mei 2012 baada ya kupatikana na makosa ya kufadhili kundi la Lashkar-e-Islam lililopigwa marufuku.

Alihukumiwa pia kifungo cha miaka 33 jela kwa madai ya kushirikiana na kundi hilo na mahakama moja ya kikabila, ijapokuwa hukumu hiyo ilipunguzwa na kufikia miaka 23 baada ya kukata rufaa.

Daktari huyo pia alishutumiwa kwa kutoa msaada wa dharura kwa wapiganaji hao na kuyaruhusu makundi kama hayo katika hospitali ya serikali aliyokuwa akisimamia.

Akiwa kifungoni, daktari huyo alifanikiwa kupeleka barua aliyoandika kwa mkono kwa wakili wake akisema kwamba ananyimwa haki.