Daraja la Kigongo – Busisi Tanzania kuweka historia kwa urefu Afrika Mashariki na Kati

Muktasari:

Shughuli hii ni miongoni mwa mambo kadhaa yanayoanza kutekelezwa na viongozi wa Kitaifa kuadhimisha miaka 58 ya Uhuru wa Tanganyika. Daraja hilo litajengwa kwa miezi 48 na kugharimu Sh700 bilioni.

Mwanza. Yawezekana watu wakisikia taarifa za Rais wa Tanzania, John Magufuli kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja la Kigongo-Busisi unadhani ni daraja la kawaida kama madaraja mengine nchini.

Wanaodhani hivyo wanajidanganya kwa sababu utakapokamilika, daraja hilo linalounganisha Wilaya za Misungwi na Sengerema za Mkoa wa Mwanza nchini Tanzania pamoja na mikoa ya Mwanza na Geita litakuwa ndilo daraja refu kuliko lote katika Ukanda huu Afrika Mashariki na Kati.

Daraja hilo linaunganisha barabara zinazoenda nchi jirani za Uganda, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Daraja hilo ambalo ujenzi wake utagharimu zaidi ya Sh700 bilioni kwa mujibu wa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mwasiliano, Isaac Kamwele, litakuwa na urefu wa kilomita 3.2 likipita juu ya Ziwa Victoria.

Mradi huo pia utahusisha ujenzi wa barabara unganishi wenye urefu wa Kilomita 1.6 na fedha zote za utekelezaji zinatokana na mapato ya ndani.

Alipotangaza uamuzi wa kujenga daraja eneo hilo wakati wa ziara zake kadhaa mkoani Mwanza, Rais Magufuli alisema kukamilika kwa mradi huo siyo tu kutarahisisha usafiri na usafirishaji, bali pia utaondoa adha ya wagonjwa kupoteza maisha wakati wakisubiri vivuko vinavyotoa huduma eneo hilo.

Eneo la Kigongo – Busisi linahudumiwa na vivuko viwili vya Mv Mwanza ambacho ni kipya na Mv Misungwi ambazo hutumia wastani wa dakika 30 hadi 40 kuvuka kutoka upande mmoja hadi mwingine.

“Kila siku watu wamekuwa wakisubiri feri (kwa muda mrefu) haiwezekani kila siku tunategemea feri. Anafika pale mama mjamzito mpaka ukasubiri feri; uchungu utakusubiri wakati mtoto anataka atoke? Pale wameshakufa watu.” amewahi kukaririwa akisema Rais Magufuli

“Tumeomba fedha kutoka kwa wafadhili tumekosa. Tumeamua tunajenga kwa fedha zetu wenyewe,”

Tayari Rais Magufuli na viongozi wengine wa Kitaifa, kidini na wananchi wamewasili eneo la tukio.