Dk Bashiru aeleza mkakati kumng’oa Zitto Kabwe Kigoma Mjini

Sunday January 19 2020

 

By Happiness Tesha, Mwananchi [email protected]

Kigoma. Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amesema chama hicho tawala nchini Tanzania kinajipanga kuibuka na ushindi wa ubunge katika jimbo la Kigoma Mjini linaloongozwa na Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo).

Mwaka  2010 hadi 2015 mbunge wa Kigoma Mjini alikuwa Peter Serukamba wa CCM ambaye katika uchaguzi wa mwaka 2015 alikwenda kugombea jimbo la Kigoma Kaskazini huku Zitto ambaye alikuwa mbunge wa jimbo hilo akienda kugombea Kigoma Mjini.

Katika maelezo yake,  Dk Bashiru amesema wapo tayari kulirejesha jimbo hilo mikononi mwa CCM kwa gharama zozote katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Oktoba, 2020.

Akizungumza leo Jumapili Januari 19, 2020 manispaa ya Kigoma Ujiji katika mkutano na wanachama wa CCM na kugawa vitambulisho kwa mabalozi, Dk Bashiru amesema jimbo hilo kwa muda mrefu limekuwa mikononi mwa wapinzani.

"Sababu tunayo, nia tunayo na malengo tunayo hakuna atakayeweza kuturudisha nyuma kwa kasi yetu tunayoendana nayo," amesema Dk Bashiru.

Amesema Serikali imefanya mambo mbalimbali ya maendeleo na wananchi wanajua, kwamba hawawezi kuwachagua tena wapinzani.

Advertisement

 

Advertisement