Hatima maombi ya Tundu Lissu kutetea ubunge wake kuamuliwa Jumatatu

Muktasari:

Mahakama Kuu ya Tanzania Jumatatu ya Agosti 26,2019 itatoa uamuzi wa pingamizi lililowekwa na Serikali ya nchi hiyo dhidi ya maombi ya aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu anayeomba kibali cha kufungua kesi kupinga kuvuliwa ubunge wake na Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai.

Dar es Salaam. Hatima ya kuendelea au kukoma kwa safari ya aliyekuwa  mbunge wa  Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu kupigania kurudishiwa ubunge wake alioupoteza, kwa njia za kisheria mahakamani sasa itajulikana keshokutwa Jumatatu Agosti 26,2019 wakati Mahakama Kuu itakapotoa uamuzi wa pingamizi la awali la Serikali.

Uamuzi huo unaotarajiwa kutolewa na Jaji Sirilius Matupa ndio utakaoamua ama kuendelea na haraka zake katika hatua zinazofuata, iwapo Jaji Matupa atatupilia mbali hoja zote za pingamizi la Serikali au harakati zake kuishia hapo iwapo atakubaliana na hoja zote za pingamizi la Serikali.

Lissu amefungua maombi Mahakama Kuu, Masjala Kuu, Dar es Salaam chini ya hati ya dharura, kupitia kwa kaka yake Alute  Mughwai, ambaye amempa mamlaka ya kisheria kufanya hivyo, ikiwa ni hatua ya awali kabisa ya kupigania kurudishiwa ubunge wake.

Katika maombi hayo namba 18 ya mwaka 2019, dhidi ya Spika wa Bunge la Tanzania na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Lissu anaomba kibali cha kufungua shauri la maombi maalum kwa lengo la kupata amri mbalimbali kuhusiana na uamuzi huo wa kuvuliwa ubunge.

Amri hizo kwa mujibu wa hati ya maombi na hati ya maelezo yake ni pamoja na Mahakama kumwamuru Spika wa Bunge Job Ndugai awasilishe mahakamani taarifa ya kumvua ubunge aliyoitoa bungeni ili iweze kuupitia na kisha iamuru kuutengua na kuutupilia mbali.

Nyingine ni mahakama imwamuru Spika ampatie yeye Lissu nakala ya taarifa ya kumvua ubunge, amri ya  kusitishwa kuapishwa kwa mbunge mteule wa jimbo hilo, Miraji Mtaturu wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Maombi hayo yalikuwa yamepangwa kusikilizwa jana Ijumaa Agosti 23, 2019, lakini yalikwama baada ya Serikali ya Tanzania kupitia kwa AG, ambaye ndiye mjibu maombi wa pili, kuibua pingamizi la awali akiiomba mahakama iyatupilie mbali maombi hayo bila hata kuyasikiliza.

Katika pingamizi hilo la awali, Serikali ya Tanzania iliwasilisha jumla ya hoja nane, ikipinga kusikilizwa kwa maombi hayo kwa madai kuwa yana kasoro za kisheria.

Kutokana na pingamizi hilo la awali, mahakama imelazimika kusimamishwa usikilizwaji wa maombi ya Lissu na kusikiliza kwanza, pingamizi hilo la AG, kama ulivyo utaratibu wa kawaida, ambalo lilisikilizwa mpaka saa mbili usiku.

Jaji Matupa baada ya kusikiliza hoja za pande zote aliahirisha shauri hilo na akapanga kutoa uamuzi wake Jumatatu ya Agosti 26, saa nane mchana.

Katika hoja za pingamizi la awali la Serikali kuna hoja ambazo kama Jaji Matupa atakubaliana basi atayatupilia mbali tu maombi hayo lakini Lissu anaweza kurudisha tena baada ya kurekebisha kasoro ambazo mahakama itaziainisha.

Lakini kuna hoja nyingine za pingamizi ambazo kama mahakama itakubaliana nazo basi maombi hayo yatafutwa kabisa na Lissu atakuwa hana nafasi ya kuyarudisha tena, isipokuwa anaweza kukata rufaa Mahakama ya Rufani kupinga uamuzi huo na kisha akasubiri uamuzi wa Mahakama ya Rufani.

Lakini kama Jaji Matupa atatupilia mbali hoja zote za pingamizi la Serikali, basi Lissu sasa ataingia katika hatua nyingine ambayo ni usikilizwaji sasa wa hoja zake za kuomba kibali cha kufungua shauri kupinga kuvuliwa ubunge wake huo na majibu ya Serikali.

Kisha mahakama baada ya kutafakari na kuchambua hoja za pande zote itatoa uamuzi, iwapo Lissu ametoa hoja za kuishawishi kupewa kibali hicho au la. Kama itaridhia na hoja za Serikali kuwa hoja zake hakidhi matakwa ya kisheria kupewa hicho kibali basi maombi yake yatatupiliwa mbali.

Kama mahakama itakubaliana na hoja zake, basi itampa kibali na ndipo sasa Lissu atafungua shauri rasmi la kupinga ubunge wake kukoma na kuomba amri hizo alizozianisha.

Katika hatua hiyo pia bado Serikali inaweza kupinga usikilizwaji wa hoja zake za kupinga kuvuliwa ubunge ambalo nalo itabidi litolewe uamuzi wa kulikubali au kulikataa, kabla ya kuendelea na usikilizwaji wa hoja za msingi za kupinga kuvuliwa ubunge huo.

 

 

Mwanasheria huyo Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), yuko nchini Ubelgiji, kwa ajili ya matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu ambao hadi sasa hawajajulikana, tangu Septemba 7, 2017, aliposhambuliwa, katika makazi yake, jijini Dodoma akitokea bungeni.

Juni 28, 2019, wakati akiahirisha mkutano wa 15 wa Bunge, Spika Ndugai alitangaza kukoma kwa ubunge wa Lissu huku akisema si yeye aliyemvua ubunge bali ni matakwa ya Katiba ya Nchi.

Alitaja sababu za uamuzi huo kuwa ni kutokuhudhuria vikao vya bunge kwa muda mrefu bila kumjulisha Spika kwa maandishi mahali aliko na kutokuja taarifa za mali na madeni kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.