Iran yaruhusu wanawake kuingia uwanjani kwa mara ya kwanza, wakishinda 14-0

Muktasari:

Tangu mwaka 1979 wanawake walikuwa hawaruhusiwa kuingia uwanjani kwenye mechi za soka za wanaume hadi hapo Alhamisi walipoishuhudia timu yao Iran ikiishinda Cambodia mashindano kufuzu Kombe la Dunia 2022.

MAELFU ya mashabiki wanawake wa mchezo wa soka huko Iran walipeperusha bendera wakishangilia na kupiga kelele kusherehekea baada ya kuruhusiwa kuingia uwanjani kushuhudia mechi kwa mara ya kwanza baada ya miongo kadhaa.
Mashabiki hao wanawake waliruhusiwa kuingia uwanjani wakati timu yao ya taifa, Iran ilipomenyana na Cambodia katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2022 zitakazofanyika Qatar. Mechi hiyo ilifanyika kwenye Uwanja wa Azadi huko Tehran.
Iran ilitenga tiketi 4,000 za mashabiki wa kike kuingia uwanjani katika mechi hiyo, ambayo Iran walishinda mabao 14-0, wakifunga mara saba hadi kufikia mapumziko. Shikirisho la kimataifa la vyama vya mchezo wa soka (Fifa) kwa muda mrefu limekuwa likiishinikiza Iran kuruhusu wanawake kuingia viwango kwenye mechi za soka ili kushangilia. Wanawake walikuwa wakipigwa marufuku kwenda viwanjani kwenye mechi za soka tangu mwaka 1979 baada ya mapinduzi ya kiislamu, lakini sasa Alhamisi zaidi ya mashabiki wa kike 3,500 waliingia uwanjani kushuhudia mechi ya soka iliyocheza kwenye uwanja wenye uwezo wa kuingiza watazamaji wanaoketi 78,000.
Picha zilizopigwa uwanjani hapo ziliwaonyesha wanawake wakiwa kwenye furaha kubwa wakipeperusha bendera za Iran na kushangilia timu yao iliyotoka uwanjani na ushindi huo mnono wa mabao 14-0.
"Tulifurahia kwa saa tano. Sote tulikuwa na furaha, tukicheka na wengine walilia kwa furaha," aliandika mwanamke mmoja wa Kiiran kwenye ukurasa wake wa Twitter.
"Hiki kitu tumechelewa sana kukifanya kwelie maisha yetu, lakini ninafuraha kwa sababu wasichana wadogo wamekuja uwanjani pia."
Ubaguzi wa kijinsia kuhusu wanawake kupigwa marufuku kwenye viwanja vya soka huko Iran iligusa hisia za wengi duniani baada ya mwezi uliopita, mwanamke mmoja aliyetambulika kwa jina la Sahar Khodayari, aliyefahamika kama 'blue girl' kutokana na timu ya soka aliyokuwa akishabikia, alijichoma moto nje ya mahakama alipokuwa akisubiri hukumu ya kuhusu kuhudhuria mechi za soka kama ilivyo kwa wanaume. Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 29 alifariki wiki moja baadaye. Fifa iliingilia kati na kuishinikiza Iran kuruhusu wanawake kwenye viwanja vya soka.
Mwaka jana, Saudi Arabia ilitoa ruhusa ya wanawake kwa mara ya kwanza kwenda kuhudhuria mechi za soka za wanaume kitu ambacho huko nyuma kulikuwa kikizuiliwa.