VIDEO: Jacqueline Mengi adai kuzuiwa kutembelea kaburi la mumewe

Moshi. Miezi tisa baada ya kifo cha mfanyabiashara Reginald Mengi, mkewe Jacqueline Ntuyabaliwe Mengi amelalamikia kile alichodai kuwa ni kitendo cha kuzuiwa yeye pamoja na wanaye wawili kutembelea kaburi na mumewe.

Kupitia ukurasa wa mtandao wake wa kijamii wa Twitter, Jacqueline alieleza malalamiko yake hayo huku akisisitiza kuwa amechoka. “Nimechoka, sitakubali kuendelea kuona wanangu wakisononeka na sitakaa kimya,” unasomeka ujumbe huo.

Mengi, aliyekuwa mmiliki wa Kampuni ya IPP inayomikili vyombo vya habari vya ITV/Redio One na The Guardian Limited, alifikwa na mauti usiku wa kuamkia Mei 2, mwaka jana akiwa Dubai, Falme za Kiarabu.

Mengi ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (Moat) alizikwa Mei 9, 2019 nyumbani kwake Nkuu Sinde, Machame mkoani Kilimanjaro.

Katika ujumbe wake huo Jacqueline amesisitiza, “nimenyamaza kwa mengi sana tu. Mmefikia hatua ya kunizuia mimi na wanangu kuingia kwenye kaburi la mume wangu, tunafukuzwa eti mpaka tuombe ruhusa ya kuingia kwenye kaburi la mume na baba wa watoto wangu!”

Hata hivyo, Benjamin Mengi ambaye ni mdogo wa Mengi alipoulizwa kuhusu madai hayo alisema hana taarifa hiyo na kwamba wakati huo (jana mchana) alikuwa msibani, “hiyo habari sijaisikia na sina habari za namna hiyo kabisa. Nipo kwenye kilio,” alisema Benjamin.

Akizungumza na gazeti hili jana, Jacqueline alikiri kuandika ujumbe huo kupitia Tweeter na kwamba amefanya hivyo kutokana na kile alichofanyiwa juzi mchana kuzuiwa kuingia katika eneo alikozikwa mumewe.

“Ilikuwa ni jana (juzi) mchana nilikuwa Moshi kushiriki msiba wa ndugu yangu na tulipotoka nilikwenda nyumbani ili kuweka maua kwenye kaburi la mume wangu. Nilikuwa na dada yangu, watoto wangu, dereva na mlinzi,” alisema Jacqueline na kuongeza:

“Tulipofika pale nyumbani dereva alipiga honi kwa sababu geti lilikuwa limefungwa. Mlinzi alitoka kutuuliza sisi ni akina nani na mimi nilijitambulisha na kuwambia kwamba nakwenda kwenye makaburi kuweka maua”.

Alisema baada ya kujitambulisha, mlinzi alisema hawezi kuwaruhusu kuingia katika eneo hilo hadi wapate ruhusa kutoka kwa Benjamin Mengi.

“Baada ya kauli hiyo ulitokea mzozo mkubwa kiasi cha kuwavuta majirani, na baada ya mzozo huo tuliingia ndani na kukuta eneo la makaburi limefungwa kwa kufuli,” alisema.

“Hebu fikiria, ni lini makaburi ya familia yakafungwa kwa kufuli, mimi siwezi kukubali eti eneo alikozikwa mume wangu mtu anizuie kwenda, huo sio ubinadamu”.

Jacqueline alikiri kutokuwa na uhusiano mzuri na familia ya mumewe akisema ni kutokana na maneno mabaya waliyoyaandika kwenye hati ya kiapo dhidi ya Mzee Mengi, katika kesi ya kupinga wosia ulioachwa na marehemu.

Hata hivyo hakuwa tayari kusema ni maneno gani na badala yake alisema yanaweza kupatikana kwenye nyaraka za kesi zilizoko Mahakama Kuu masjala ya Dar es Salaam.

Jacqueline ni mke wa pili wa Marehemu Regnald Mengi. Mke wa kwanza ni Marehemu Mercy Mengi ambaye kabla ya kifo chake alikuwa ametalikiwa.