Jaji Mutungi: Sheria haimzuii aliyehama chama kugombea uongozi

Muktasari:

Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Mutungi amesema sheria ya marekebisho ya sheria ya Vyama Siasa ya mwaka 2019 imeanza kutumika rasmi huku akiwataka wananchi kupuuzia taarifa zinazosambazwa kwamba mwanachama akihamia chama kingine ni lazima akae miaka miwili ili agombee.

Dar es Salaam. Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania, Jaji Francis Mutungi amesema Sheria ya marekebisho ya Sheria ya Vyama Siasa ya mwaka 2019 imeanza kutumika rasmi.

Sheria hiyo ilitungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano, Januari 2019 kisha kusainiwa na Rais John Magufuli Februari 13, mwaka huu na baadaye kutangazwa katika Gazeti la Serikali Februari 22.

Taarifa iliyotolewa leo Ijumaa Aprili 5, 2019 na Jaji Mutungi kwa vyombo vya habari imesema kila mwananchi na wadau wakuu wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa kuisoma na kutekeleza sheria hiyo inayopatikana kwenye tovuti Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.

Katika hatua nyingine, Jaji Mutungi amewataka wananchi  kupuuzia taarifa za uongo zinazosambazwa ya kwamba mwanachama akihama chama na kuhamia kingine lazima akae miaka miwili ili agombee katika uchaguzi wowote unaohusisha wanachama wa vyama vya siasa.

“Ukweli ni kwamba, Sheria ya Vyama vya Siasa na kanuni zake, haina kifungu chochote kinachoweka masharti kwa mwanachama wa chama cha siasa kuhama kutoka chama kimoja kwenda kingine,” amesema Jaji Mutungi.