Mafundi sanifu wataka kada hiyo kutambulika kielimu

Baadhi ya mafundi sanifu wakiwa kwenye mkutano mkuu wa sita wa mwaka 2024 Jijini Dodoma. Picha na Rachel Chibwete

Muktasari:

  • Wataka mfumo wa utumishi unaotambua ujuzi na uzoefu wa mafundi sanifu kutoa fursa kwao kujiendeleza ndani ya kada yao hadi kufikia ngazi ya shahada za uzamili na uzamivu

Dodoma. Mafundi sanifu nchini wameiomba Serikali kuitambua kada hiyo kwenye ngazi ya shahada za uzamili na uzamivu wakieleza wanalazimika kubadilisha fani kwenda kwenye uhandisi ili kujiendeleza kielimu.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), Menye Manga leo Alhamisi Mei 23, 2024 kwenye mkutano mkuu wa sita wa mafundi sanifu nchini uliofanyika jijini Dodoma.

Wameomba kuunda mfumo wa utumishi unaotambua ujuzi na uzoefu wa mafundi sanifu ili kutoa fursa kwao kujiendeleza ndani ya kada yao hadi ngazi hiyo ya elimu kama ilivyo kwa wauguzi.

Amesema kwa hali ilivyo sasa hakuna ngazi ya juu ya elimu kwa mafundi sanifu, hivyo wanalazimika kubadili fani kwenda kwenye uhandisi ili waweze kupanda vyeo.

“Hivi sasa tumeamua kuwekeza katika mafunzo ya maendeleo kwa mafundi sanifu, maboresho yatakayosaidia kufikia uwezo wao kamili na kuchangia ufanisi zaidi katika uchumi wa Taifa kwa kuanzisha mradi wa Jenga kesho iliyo bora (BBT) kwenye kada ya ufundi sanifu ili tuwapate vijana wengi zaidi kwenye kada hiyo,” amesema.

Fundi sanifu kutoka mkoani Geita, Kesia Kazimoto amesema wengi wao hawawezi kujiendeleza kielimu kwa sababu kada hiyo hairuhusu na ndiyo maana wanakimbilia kwenye uhandisi.

Amesema wanafanya kazi kubwa ambazo hata wenye vyeti vya darasani hawawezi huko kwenye halmashauri lakini hawatambuliki kwa kuwa si wahandisi.

Kutokana na hilo, ameiomba Serikali kufungua wigo wa mafundi hao kujiendeleza kielimu.

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameitaka Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) kuwasajili mafundi sanifu kwenye vikundi ili wapate kazi ndogondogo zinazotolewa na halmashauri badala ya kumwachia mkandarasi mmoja kazi zote,  ambazo mwisho wa siku anashindwa kuzikamilisha kwa wakati

Bashungwa amesema fedha nyingi zinazotolewa na Serikali zinakwenda kwenye halmashauri za miji, manispaa na majiji kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ya wananchi lakini huko hakuna wahandisi wa kutosha wa kutekeleza miradi hiyo.

“Unakuta halmashauri ina mhandisi mmoja anakuwa na miradi zaidi ya 50, changamoto inakuja kwenye ukamilishaji wa miradi hiyo, hivyo waunganisheni mafundi sanifu kwenye vikundi vitakavyosajiliwa ili wapewe kazi hizo na wazikamilishe kwa wakati na ubora uliokusudiwa,” amesema.

Amesema Serikali inakopa fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo kama watekelezaji watatoka nje ya nchi ina maana hakutakuwa na faida.

Pia ameitaka bodi hiyo kuwawajibisha wakandarasi ambao hawafanyi vizuri kwenye kazi zao.

“Unakuta ujenzi wa karavati unahitaji nondo nene lakini mhandisi anaweka nondo nyembamba kama ile ya kujengea mabanda ya kuku, huyo hatufai hata kidogo, hivyo anzeni kuwajibishana ninyi wenyewe huko kwenye bodi yenu,” amesema.

Msajili wa Bodi ya Mafundi Sanifu, Bernard Kavishe amesema mafundi sanifu waliopo wanaweza kutumika kwa ajili ya kuziba mapengo kwenye shule zenye upungufu wa walimu kwenye masomo ya sayansi kama vile sanyansi, hesabu, kemia, fizikia, kompyuta na jiografia kwani wengi wao wamesomea masomo hayo.

Amesema bodi hiyo imefanya ziara kwenye halmashauri 13 na mikoa miwili ya Geita na Kagera kujionea upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi kwenye shule za sekondari.

Amesema wapo kwenye mazungumzo na Serikali ili mafundi hao waweze kuziba upungufu wa walimu hao kwa makubaliano maalumu.