Jina la Waziri Mkuu Majaliwa lawatia matatani, washtakiwa kwa utakatishaji

Friday February 14 2020

 

By Pamela Chilongola, Mwananchi

Dar es Salaam. Watu watatu wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka saba likiwemo la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu zaidi ya Sh22.9 milioni kwa kutumia jina la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Washtakiwa hao ni Bahati Malila ni mjasiriamali,Regina Mamba ambaye ni mfanyabiashara na  Gogfrey Mtonyi maarufu ‘Tumaini’ ni mchapishaji wa eneo la Mbezi Beach Jogoo.

Washtakiwa hao wamefikishwa mahakama hapo leo, Februari 14, 2020 na kusomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Godfrey Isaya.

Akisoma mashtaka hayo Wakili wa Serikali Mwandamizi Mkunde Mshana alidai kuwa washtakiwa hao wanakabiliwa na shtaka la kuongoza genge la uhalifu, mawili ni ya gugushi, mawili ya kutoa nyaraka za uongo, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu  na utakatishaji wa fedha zaidi ya kiasi cha Sh22.9 milioni.

Mshana alidai  kati ya Januari 3,2020 na Januari 31,2020 washtakiwa kwa pamoja wakiwa jijini Dar es Salaam waliongoza genge la uhalifu huku wakijua kufanya hivyo ni kosa la kisheria.

Shtaka la pili kati ya Januari 14, 2020 washtakiwa hao kwa pamoja wakiwa maeneo ya Msasani wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam walighushi cheti cha mchango kwa nia ya udanganyifu waliyoghushi Januari 13, 2020 ikionyesha cheti halali kilichotolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa huku wakijua siyo kweli.

Advertisement

Katika shtaka la tatu, imedaiwa kati ya Januari 14, 2020 maeneo ya Msasani washtakiwa hao kwa pamoja walishirikiana kutoa cheti cha mchango waliyoghushi Januari 13, 2020 ikionyesha cheti halali kilichotolewa na Waziri Mkuu, Majaliwa huku wakijua si kweli.

 

Shtaka la nne kati ya Januari 14,2020 maeneo ya Masaki washtakiwa kwa pamoja walishirikiana kutoa nyaraka kwa Guanhui Su Biaolin Tang huku wakijua nyaraka hiyo ni ya uongo ambayo waliighushi Januari 13,2020 ikionyesha cheti halali kilichotolewa na Waziri Mkuu Majaliwa.

Katika tarehe hiyohiyo maeneo ya Msasani, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa walishirikiana kuwasilisha cheti cha kughushi cha mchango kwa Guanhui Su Biaolin Tang, huku wakiaminisha cheti hicho kimetolewa na Waziri Mkuu Majaliwa.

Mshana alidai katika shtaka la sita tarehe hiyohiyo maeneo ya Msasani washtakiwa hao wakiwa na lengo la kufanya ulaghai walijipatia Dola za Kimarekani 10,000 sawa na zaidi ya Sh22.9 milioni kwa Guanhui Su Biaolin Tang wakijifanya fedha hizo ni msaada wanapeleka kwa  Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Shtaka la mwisho la utakatishaji wa fedha kati ya Januari 14, 2020 maeneo ya Msasani washtakiwa wote kwa pamoja walijipatia Dola za Kimarekani 10,000 sawa na zaidi ya Sh22.9 milioni huku wakijua fedha hizo ni zao tangulizi la kughushi na kuongoza genge la uhalifu huku wakijua kufanya hivyo ni kosa la kisheria.

Washtakiwa hawakutakiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.

Upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na washtakiwa hao wamerudishwa rumande hadi Februari 28, 2020 itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.

 

Advertisement