KESI YA KINA KITILYA: Serikali yapewa sharti kuongeza shahidi

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, imeridhia maombi ya upande wa mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili Harry Kitilya na wenzake, kuongeza shahidi ambaye hakuwepo kwenye orodha yao.

Jaji Immaculata Banzi anayesikiliza kesi hiyo alifikia uamuzi huo baada ya upande wa mashtaka kuomba kumwita shahidi huyo ambaye hakuwemo katika orodha ya mashahidi wake, licha ya upande wa utetezi kupinga ombi hilo.

“Mahakama inakubaliana na taarifa ya upande wa mashtaka kumuita shahidi wa nyongeza kwa masharti wawasilishe mahakamani taarifa iliyofanyiwa marekebisho kwa kuweka wazi nyaraka ambazo shahidi huyo atakuja kuzitolea ushahidi,” alisema Jaji Banzi na kuongeza: “Taarifa hiyo iwasilishwe mahakamani kesho (leo) kabla au saa sita mchana na upande wa utetezi wapewe nakala. Shauri hili linaahirishwa hadi Julai 18, mwaka 2019 (kesho). Washtakiwa mtaendelea kuwa mahabusu.”

Mbali na Kitilya ambaye ni Mkurugenzi kampuni ya Enterprise Growth Market Advisors Limited (Egma), washtakiwa wengine ni Shose Sinare, Sioi Solomon, Bedason Shallanda na Alfred Misana.

Shallanda na Misana walikuwa watumishi wa Serikali Wizara ya Fedha.

Washitakiwa wanakabiliwa na mashtaka 58, yakiwemo ya kuisababishia Serikali hasara ya Dola 6 milioni, kujipatia fedha kiasi hicho kwa udanganyifu na utakatishaji fedha kiasi hicho, kughushi, kuwasilisha nyaraka za uongo, kuongoza uhalifu na kudanganya mwajiri.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Februari 2012 na Juni 2015 jijini Dar es Salaam na nje ya nchi wakati wa mchakato kuiwezesha Serikali kupata mkopo wa Dola za Marekeni 550milioni kutoka Benki ya Standard ya Uingereza na Stanbic Tanzania .

Serikali inadai kuwa washtakiwa walishirikiana kupanga uhalifu kwa kughushi barua ya Standard Bank na Stanbic, kuonyesha kwamba zilifanya marekebisho katika vigezo na masharti hususan ada ya uwezeshaji wa mkopo huo kutoka asilimia 1.4 hadi asimilia 2.4 ya mkopo halisi.

Jana baada ya shahidi wa sita kutoa ushahidi, Wakili wa Serikali Mkuu, Oswald Tibabyekomya aliieleza mahakama kuwa washawasilisha mahakamani taarifa ya kusudio la kuita shahidi kutoka Dodoma.

Alisema walibaini umuhimu wa shahidi huyo Ijumaa wakati shahidi wa tatu akitoa ushahidi wake na kwamba tayari shahidi huyo alikuwa ameshaanza safari kuja jijini Dar es Saalam.

Kiongozi wa jopo la mawakili wa utetezi, Dk Masumbuko Lamwai alipinga maombi hayo pamoja na mambo mengine akidai kuwa ingawa upande wa mashtaka wana haki hiyo kisheria lakini hawana budi kukidhi matakwa ya kisheria hasa kifungu cha 289 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).

Dk Lamwai alidai kuwa wanapaswa waeleze ni lini walibaini kiini na umuhimu wa ushahidi wa shahidi huyo, wapewe nyaraka atakazokuja kuzitolea ushahidi ili wawe katika nafasi nzuri ya kumhoji.

Pia, Dk Lamwai alipinga maombi ya upande wa mashtaka kuomba kesi hiyo iahirishwe hadi leo mchana, wapate fursa ya kumuandaa shahidi wanayetaka kumwongeza, badala ya asubuhi. Alidai huo ni ucheleweshaji wa mwenendo wa kesi hiyo ambao umekuwa ukifanywa na upande wa mashtaka, akaiomba mahakama iamuru waendelee na shahidi mwingine badala ya kusubiri huyo ambaye hata hivyo hawajakidhi matakwa ya kisheria kumwita.

Akijibu hoja hizo Wakili Tibabyekomya alidai taarifa imebainisha kiini cha ushahidi wa shahidi huyo na iliwasilishwa mahakamani na mawakili wa utetezi walipewa kwa wakati.

Kuhusu madai ya kuchelewesha kesi alidai hawana nia hiyo bali nia yao ni kuona kesi inamalizika haraka, lakini akasisitiza kuwa wana jukumu la kuthibitisha mashtaka bila kuacha mashaka yoyote, hivyo wana haki kuandaa na kuendesha kesi yao ili iishe vizuri.

Awali shahidi huyo wa sita, Neema Chelelo aliieleza mahakama kuwa mwaka 2012 alikuwa akifanya kazi Wizara ya Fedha na Uchumi, Idara ya Sera akiwa mwandishi mwendesha ofisi, ofisi ya Mkurugenzi Msaidizi wa Sera, Kitengo cha Madeni.

Alidai kuwa Agosti 6, mwaka huo alipokea barua iliyonesha kuwa imetoka Benki ya Standard ikipendekeza kuiwesha Serikali ya Tanzania kupata mkopo wa Dola za Marekani 550 milioni akampelekeza mkuu wake ilimaifanyie kazi, mshtakiwa wa tano, Misana.

Shahidi huyo alidai kuwa baada ya hapo barua hiyo haikurudi kwake na hakuiona tena hadi alipokwenda kuhojiwa na Takukuru mwaka 2016 ndipo akaonyeshwa huko.