Kafulila awajia juu wanaotafuna michango

Katibu tawala Mkoa wa Songwe, David Kafulila

Muktasari:

Katibu tawala Mkoa wa Songwe amewakalia kooni watendaji wanaotafuna fedha za makusanyo baada ya kuzikusanya badala ya kuziwakilisha benki

 

Mbozi. Katibu tawala Mkoa wa Songwe, David Kafulila amewaagiza wakurugenzi watendaji wa halmashauri kuwachukulia hatua kali za kiutumishi watumishi wanaotafuna fedha za makusanyo kabla hawajachukuliwa hatua wao.

Kafulila ameitoa kauli hiyo leo, Jumanne Februari 18 mwaka huu katika kikao cha kamati ya ushauriano cha mkoa (RCC) kuwa halmashauri zinakwama kufikia malengo ya makusanyo kutokana na wakusanyaji hao kula fedha baada ya kuzikusanya badala ya kuziwasilisha benki.

"Wakusanyaji wa mapato ya halmashauri ni watumishi wa umma, wanatambua kuwa ulaji wa fedha za Serikali ni kosa ambalo linatosha kumfukuzisha kazi mtumishi husika kwa mujibu wa kanuni na kuchukua hatua nyinginezo za kisheria," amesema Kafulila.

Kafulila alitangaza kupiga marufuku kufanya majadiliano na watumishi aliodai ni wezi na kutoa siku saba hatua ziwe zimechukuliwa na wahusika hao wafikishwe Takukuru.

Aidha inadaiwa kuwa zaidi ya Sh200 milioni zipo mikononi mwa watendaji ambazo zimekusanywa kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato ya halmashauri.

Mkuu wa wilaya Momba, Jumaa Said Irando amesema katika wilaya yake zaidi ya Sh63 milioni zipo mikononi mwa watendaji na kuwa orodha yake ameiwasilisha Takukuru.