Kamati ya Bunge yalia na ongezeko la ukatili nchini

Muktasari:

Kamati ya Bunge la Tanzania ya Huduma na Maendeleo ya Jamii imewasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli zake, huku ikisema kuna ongezeko kubwa la vitendo vya ukatili nchini.

Dodoma. Kamati ya Bunge la Tanzania ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, imesema kumekuwa na ongezeko la matukio ya ukatili wa kijinsia nchini hususan kwa wanawake na watoto.

Matukio hayo sasa yamefikia 43,487 mwaka 2018 kutoka watu 31,996 mwaka 2016.

Akiwasilisha taarifa ya Kamati hiyo leo Alhamisi Februari 6, 2020 bungeni Jijini Dodoma, Mwenyekiti wa kamati hiyo Peter Serukamba amesema ongezeko hilo ni la asilimia 35.9.

“Madhara yanayotokana na ukatili huo ni makubwa ikiwemo kuumizwa vibaya, kupata ulemavu wa viungo, madhara ya kisaikolojia na hata kupoteza maisha kwa baadhi ya watu,” amesema Serukamba.

Amesema kutokana na hilo, Kamati hiyo inashauri Serikali kuweka utaratibu wa kuzishauri halmashauri kutenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa uhamasishaji wa namna bora ya kupunguza ukatili huo na hata kujikinga na kutoa taarifa katika vyombo husika ikiwemo polisi.