Kampuni ya As Salaam yazindua safari za ndege Zanzibar-Dodoma

Muktasari:

Mkuu wa Wilaya ya Bahi (DC) mkoani Dodoma nchini Tanzania, Mwanahamisi Munkunda amezindua safari za ndege kati ya Zanzibar -Dodoma kupitia Dar es Salaam huku akiwataka kuhakikisha huduma zao zinakuwa bora ikiwamo kuzingatia muda wa safari.

Dodoma. Kampuni ya Ndege ya As Salaam imezindua safari za ndege kati ya Zanzibar- Dodoma kupitia Dar ee Salaam nchini Tanzania huku Mkuu wa Wilaya ya Bahi (DC) mkoani humo, Mwanahamisi Munkunda akiitaka kampuni hiyo kuhakikisha huduma zake zinakuwa bora na zinazozingatia muda.

DC huyo aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge alitoa wito huo jana Ijumaa Januari 24,2020 wakati wa uzinduzi wa safari hizo zitakazokuwa tatu kwa wiki.

Mwanahamisi alisema safari hizo zinaonyesha jinsi kampuni hiyo inavyounga mkono juhudi za Serikali ya Tanzania na chama tawala CCM ya kuhamishia makao makuu Dodoma.

"Hii mnaonyesha Muungano wetu wa Tanganyika na Zanzibar uko imara na inatusaidia sisi viongozi kupafa usafiri wa uhakika si wa kuunga unga na hii ni safari ya kimkakati na kimaendeleo," alisema Mwanahamisi

Mkuu huyo wa Wilaya alisema, "sasa tutapata karafuu moja kwa moja na kwa wakati kutoka Zanzibar na wafanyabiashara wa Dodoma watapata fursa ya kutoa mvinyo Dodoma hadi Zanzibar na sisi viongozi tutawaunga mkono."

Alisema abiria anayetoka Mwanza anafika Dodoma anaunga kwenda Zanzibar na yule anayetoka Arusha kwa gari akifika hapa anaunga kwenda Zanzibar.

"Sisi kama viongozi tutawasaidia kuwaletea wateja na mmewasaidia sana sana wabunge wetu wa Zanzibar, watoke hapa hadi Dar es Salaam kisha wakaunga Zanzibar lakini sasa kutakua na usafiri wa moja kwa moja," alisema

"Hii ndiyo Rais wetu anataka, kufungua fursa kama hizi na sasa tutapata huduma na vifaa mbalimbali kutoka Zanzibar bila kukawia Dar es Salaam."

Mkuu huyo wa Wilaya alitumia fursa hiyo kuitaka kampuni hiyo kuhakikisha wanazingatia muda ili kuepusha malalamiko kutoka kwa wateja wao pindi wanapocheleweshewa usafiri kulingana na walivyoahidiwa.

"Mnafahamu katika biashara muda ni kila kitu na kampuni nyingi za ndege zimekuwa zikilalamikiwa, muda ni kila kitu, mtu amefika hapa saa 3 asubuhi anakaa hadi saa 6 mchana au saa 9, hakikisheni mnazingatia muda ila kujenga imani kwa wateja wenu," alisema

"Mtu anakuwa na miadi yake, kumchelewesha kutawarudisha nyuma, Dodoma saizi ni makao makuu, kwa hiyo hakikisheni hili mnalifanya lakini ongezeni safari za kila siku Dodoma hii ya Jumatatu, Jumatano na Ijumaa pekee hazitoshi," alisema

Awali, Mkurugenzi wa Biashara As Salaam, Ibrahim Bukenya alisema wameamua kuanzisha safari hizo kutokana na mahitaji na kutokuwapo usafiri wa moja kwa moja wa Zanzibar- Dodoma kupitia Dar es Salaam.

Bukenya alisema watahakikisha huduma zinakuwa bora na wanazingatia muda ili kuongeza wigo wa biashara kati ya maeneo hayo muhimu hasa ikizingatiwa Dodoma ni makao makuu.

Mmoja wa abiria Ibrahim Abdallah alisema hatua hiyo ni nzuri na itaongesha ushindani wa kampuni za ndege katika utoaji wa huduma hasa ikizingatiwa, “hawa As Salaam wao watakuwa wana safari za moja kwa moja za Zanzibar –Dodoma ambazo hazikuwapo.”