Kesi ya DC Chemba kumtaliki mkewe yapigwa kalenda hadi Agosti 5

Mkuu wa Wilaya ya Nchemba, Simon Odunga.

Muktasari:

  • Mahakama ya Mwanzo Ukonga, Dar es Salaam Jumatatu Agosti 5, 2019 itaanza kusikiliza kesi ya madai ya talaka namba 181  iliyofunguliwa mahakamani hapo na mkuu wa Wilaya ya Nchemba, Simon Odunga

Dar es Salaam. Mahakama ya Mwanzo Ukonga, Dar es Salaam Jumatatu Agosti 5, 2019 itaanza kusikiliza kesi ya madai ya talaka namba 181  iliyofunguliwa mahakamani hapo na mkuu wa Wilaya ya Nchemba, Simon Odunga.

Kesi hiyo ilitakiwa kuanza kusikilizwa jana Jumanne Julai 30, 2019 mbele ya Hakimu Christina Luguru lakini imesogezwa hadi Agosti  baada ya wahusika kufika mahakamani lakini hawakusikia kesi yao ilipotajwa, hivyo kushindwa kuhudhuria.

Odunga  alifunga ndoa kanisa la Sabato na kupata cheti cha ndoa  A namba 00140917.

Katika kesi nyingine ya madai ya talaka namba 180 ya 2019 iliyofunguliwa  tena mahakamani hapo na Odunga dhidi ya ndoa aliyoifunga serikalini itasikilizwa Agosti 19, 2019.

Katika kesi hiyo ya pili, Odunga anaomba  talaka ya ndoa ya Serikali aliyoifunga  Februari 21, 2010 na Ruth Osoro na kupewa cheti B namba 0979341.

Analalamikiwa  na mkewe kwa kutotoa matunzo ya mtoto wao wa kiume mwenye umri wa miaka minne kwa kipindi cha miaka mitatu.

Licha ya malalamiko hayo, Odunga anaomba mahakamani hapo  apewe ridhaa ya kumlea mtoto huyo bila kubughudhiwa.

Katika kesi hiyo ya pili, Odunga anaomba kutoa talaka kwa mkewe huyo  kwa sababu amechoshwa na ugomvi na kudhalilishwa sehemu ya kazi.

Hata hivyo, alieleza mahakamani hapo kuwa hana mashaka na malezi ya mama wa mtoto huyo na anataka kumlea mwanaye kuepuka kadhia ya kudhalilishwa kila mahali ikiwapo kazini.