Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kigogo Chadema auawa kinyama Geita

Marehemu Alphonce Mawazo enzi za uhai wake.

Muktasari:

Wananchi na wafuasi wa Chadema walifurika katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Wilaya ya Geita, wakionekana wenye nyuso za huzuni.

Geita. Mji wa Geita umezizima kwa simazi, vilio na majonzi baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Geita, Alphonce Mawazo kuuawa kinyama kwa kushambuliwa na silaha za jadi ikiwamo kukata kichwa kwa shoka.

Wananchi na wafuasi wa Chadema walifurika katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Wilaya ya Geita, wakionekana wenye nyuso za huzuni.

Mawazo (pichani) alifariki dunia baada ya kudaiwa kutekwa na kundi la watu hao wanaosadikika kuwa ni wafuasi wa chama kimoja cha siasa wakiwa na marungu, mapanga na shoka.

Kabla ya kukumbwa na mkasa huo alikuwa Katoro kwenye Kikao cha ndani kwa maandalizi ya uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Ludete, ambao umepangwa kufanyika leo baada ya kuahirishwa kutokana na vifaa vya kupigia kura kuchelewa kwenye kata hiyo.

Mashuhuda wanasema ndani ya kikao hicho kulikuwa na mtu waliyehisi kuwa ni mamluki na baada ya kumuhoji, wajumbe walianza kumpiga na ndipo kikundi cha vijana waliokuwa nje kilipoingia na kuanza mapambano.

Baada ya kuona hivyo, Mawazo alitoka na kuchukua pikipiki ili kutoroka eneo hilo, lakini alifuatwa na gari moja na walipomfikia walimkatakata kwa mapanga na kumuacha akiwa kwenye hali mbaya kabla ya kufariki.

Mbowe atoa kauli

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema chama kimepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za kifo hicho.

“Kwa niaba ya viongozi na wanachama wote wa Chadema, Mwenyekiti Mbowe ametuma salaam za pole na rambirambi kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki, wanachama wa Chadema na wote walioguswa na kifo hicho cha kikatili, akivitaka vyombo vya dola vitoe taarifa kamili ya wahusika wa unyama huo,” inasema taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Chadema jana.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo Mbowe alimuelezea Mawazo kama mmoja wa wapiganaji jasiri na makini ambao wapenda mabadiliko walikuwa wakijivunia kuwa naye.

“Hakika tumepoteza moja ya nguzo muhimu za chama Kanda ya Ziwa. Chama kimepokea kwa mshtuko mkubwa kifo hiki ambacho tunaamini kimepangwa,” anasema Mbowe katika taarifa hiyo.

“Tunavitaka vyombo vya dola vitupe taarifa kamili ya wahusika wa unyama huu. Nawapa pole wanachadema wote, ndugu na jamaa.”

Mbali ya kuwa mwenyekiti wa chama wa mkoa, Mawazo pia alikuwa mjumbe wa Baraza Kuu na mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa.

Daktari athibitisha.

Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Geita, Dk Adamu Sijaona alisema walimpokea majeruhi saa 9:00 alasiri akiwa katika hali mbaya na alikuwa hajitambui.

“Alikuwa na majeraha makubwa kichwani, katikati ya kichwa. Alikuwa amepoteza fahamu kabisa na walikuwa wamemchelewesha,” alisema Dk Sijaona.

Alisema Mawazo alifariki dunia kutokana na kuvuja damu nyingi wakati madaktari wa hospitali hiyo wakijaribu kuokoa maisha yake.

Alisema mwili wake umehifadhiwa hospitalini wakati taratibu nyingine zikiendelea.

Ilivyokuwa.

Taarifa za awali zinadai kuwa, Chadema walikuwa na mkutano wa ndani katika ukumbi wa Makungu uliopo Mtaa wa CCM mjini Katoro na baadaye walibainika kuwa kuna kijana alikuwa akirekodi mkutano huo.

Kamanda wa polisi mkoa, Latson Mponjoli hakuwa tayari kuzungumzia tukio hilo.

’’ Nipo nje ya ofisi na mimi ndiyo nafuatilia ili nipate data za kutosha kuhusiana na tukio hilo, siwezi kukueleza ni muda gani nitakuwa tayari, naomba uniache kwanza, ’’ alisema Kamanda Mponjoli na kukata simu wakati alipohojiwa na gazeti hili.