Kitabu cha maisha ya Mkapa kimeandikwa kwa miaka minne

Muktasari:

Taasisi ya Uongozi Institute kitabu cha Rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa cha Maisha Yangu, Kusudio Langu kimeandaliwa tangu mwaka 2016.

Dar es Salaam. Taasisi ya Uongozi Institute kitabu cha Rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa cha Maisha Yangu, Kusudio Langu kimeandaliwa tangu mwaka 2016.

Akizungumza leo Jumanne Novemba 12, 2019 katika uzinduzi wa kitabu hicho, ofisa mtendaji mkuu wa taasisi hiyo, Profesa  Joseph Semboja amesema walipewa jukumu la kuongoza kada ya uongozi nchini, moja ya jukumu lake ni kuandaa tawasifu za viongozi.

“Kuzindua tawasifu ya Rais mstaafu Mkapa ni mwanzo wa kuelekea sehemu nyingine ya programu hii na hivi punde tutakuwa tunasherehekea maisha ya Mwinyi (Ali Hassan- Rais wa Awamu ya pili) kitabu kipo karibu kukamilika,” amesema.

Profesa Semboja amesema kuandika vitabu kuhusu maisha ya viongozi inasaidia wengi kujifunza namna bora ya kuishi, akibainisha kuwa viongozi wengi hawaandiki vitabu kutokana na kukabiliwa na mambo mengi.

“Tunapoandika historia ya kiongozi tunaandika historia ya nchi na ndio maana imeshirikisha maisha ya Watanzania wengi, hili tukio si la kifamilia ila ni la Taifa la Tanzania,” amesema.

Amesema kitabu hicho kilianza kuandikwa mwaka 2016 na kimechukua muda mrefu kutokana na mambo mengi ya kuhakikiwa, kukutana na watu ili kukikamilisha.

Amebainisha kuwa kitabu hicho kimegharimu Sh230 milioni na kinapatikana katika maduka mbalimbali ya vitabu na mitandaoni.

“Miaka 81 iliyopita siku ya Jumamosi mkoani Mtwara alizaliwa mtoto wa kiume, leo anasherehekea siku yake ya kuzaliwa na kumshukuru Mungu kwa zawadi ya uhai.”

“Ameamua kutuzawadia kitabu sehemu ya maisha kwa historia ya maisha yetu, ameamua hatachukua hata senti moja ya mauzo ya kitabu hii faida itarudi taasisi ya uongozi,” amesema.

Kitabu hicho kina kurasa 316 na sura 16.