Komu kama Mbatia, asimamishwa kufanya kampeni

Mgombea ubunge Moshi Vijijini kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi, Anthony Komu

Muktasari:

Mgombea ubunge Moshi Vijijini kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi, Anthony Komu amesimamishwa kufanya kampeni kwa siku saba kuanzia leo Jumamosi Oktoba 17 hadi 23, 2020 baada ya kamati ya maadili ya jimbo hilo kumtia hatiani kwa kosa la kukiuka maadili ya uchaguzi mkuu.

Moshi. Mgombea ubunge Moshi Vijijini kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi, Anthony Komu amesimamishwa kufanya kampeni kwa siku saba kuanzia leo Jumamosi Oktoba 17 hadi 23, 2020 baada ya kamati ya maadili ya jimbo hilo kumtia hatiani kwa kosa la kukiuka maadili ya uchaguzi mkuu.

Mbali  na adhabu hiyo, kamati ya maadili jimbo la Moshi vijijini itakaa tena leo kujadili malalamiko mengine ya ukiukwaji wa maadili yaliyowasilishwa na mgombea ubunge wa CCM, Profesa Patrick Ndakidemi.

Komu anaingia katika orodha ya wabunge waliopewa adhabu ya kusimamishwa kufanya kampeni baada ya jana mgombea ubunge Vunjo kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi, James Mbatia kusimamishwa kufanya kampeni kwa siku saba.

Wakati Komu akisimamishwa kwa kutumia bango ambalo halijaidhinishwa na msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, Mbatia  amesimamishwa kwa kutumia kipeperushi ambacho hakijaidhinishwa na msimamizi.

Komu ameithibitishia Mwananchi kupewa adhabu hiyo lakini akasema hajakubaliana nayo na tayari anafanya mchakato wa kuwasilisha rufaa kwenye kamati ya kitaifa ya maadili ya uchaguzi mkuu.

Makosa mengine anayotuhumiwa Komu ambayo yatasikilizwa leo, ni wakala wake kufika katika mkutano wa mgombea wa CCM na gari lenye picha za Komu na kukiuka ratiba na kuingia mkutano wa mgombea huyo.