LeBron James awasha moto mzozo wa China-NBA

Muktasari:

Mchezaji huyo nyota wa NBA amemshutumu kiongozi wa Houston Rockets kwa kutuma ujumbe wa Twitter ulioiudhi China.


Los Angeles, Marekani (AFP). Nyota wa mchezo wa mpira wa kikapu, LeBron James ameshutumiwa kwa kuamua kutoona ukandamizaji nchini China baada ya kumkosoa kiongozi wa klabu ya Houston Rockets kwa kuiudhi China kutokana na kuandika ujumbe katika akaunti ya Twitter kuunga mkono waandamanaji wa Hong Kong akiwa na taarifa zilizoipotoshwa.

James alimwambia meneja mkuu wa Rockets, Daryl Morey kuwa "hakuwa ameelimishwa" kuhusu Hong Kong na alitakiwa kukaa kimya na kusababisha nyota huyo ambaye ana kawaida ya kuzungumza chochote, kuingia kwenye mzozo ambao wachezaji wenzake wa Ligi ya Mpira wa Kikapu ya Marekani (NBA) wameuepuka.

"Watu wengi wangeweza kudhurika si tu kifedha bali pia kimwili, kiakili na kiroho. Kwa hiyo kuwa makini na kile tunachotuma, na tunasema na tunafanya," James aliwaambia waandishi wa habari alipoulizwa maoni yake jijini Los Angeles baada ya kurejea kutoka katika ziara ya kila mwaka ya NBA nchini China.

Kauli yake ilisifiwa na watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini China ambao walimlaumu Morey kwa kuingilia mambo ya ndani ya nchi yao, lakini hali ilikuwa tofauti nchini Marekani.

"@KingJames — unasambaza propaganda za kikomunisti. China inaendesha kambi za mateso na unajua," alisema seneta wa chama cha Republican, Ben Sasse wa Nebraska, akimaanisha waislamu wapatao milioni moja wa Uighur wanaoshikiliwa kwenye makambi.

Mzozo uliosababishwa na kauli ya Morey uligharimu matangazo ya moja kwa moja ambayo huwa na fedha nyingi, mauzo ya bidhaa na matarajio ya udhamini katika nchi hiyo ambayo NBA ina mashabiki wengi.

Lakini NBA pia imeingia matatizoni kutoka kwa wanasiasa wa Marekani na vyombo vya habari ambao wanaitaka ligi hiyo isisalimu amri kwa China.

Baada ya maneno yake kwa waandishi wa habari, James -- ambaye ana mkataba mnono na kampuni ya vifaa vya michezo ya Nike ambayo inafanya biashara kubwa nchini China -- alijaribu kufafanua msimamo wake kwa kutuma ujumbe kadhaa katika akaunti ya Twitter.