Lowassa asema utendaji wa Magufuli umeifanya nchi kushika adabu

Muktasari:

Waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa amesema kuondolewa kazini kwa watendaji wazembe na wasiotimiza wajibu wao umefanya nchi kushika adabu.

Monduli. Waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa amesema kuondolewa kazini kwa watendaji wazembe na wasiotimiza wajibu wao umefanya nchi kushika adabu.

Lowassa ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Septemba 20, 2019  katika mahafali ya Shule ya Msingi Meyers mjini Arusha.

"Rais  Magufuli (John)  anastahili pongezi  anafanya kazi nzuri sana, tunaona mawaziri wanafanya kazi nzuri ,Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) yupo kule wengine huku nchi imewaka moto kila sehemu,” amesema.

Asema kazi nzuri za Rais zinapaswa kupakwa ‘poda’ kwa kuhusisha na kuboresha elimu ambayo itawapa ujuzi wahitimu kujiajiri.

"Kuna vijana wengi wanamaliza masomo kutokana na mpango wa elimu bure sasa tujitahidi elimu hii iwasaidie vijana kupata ujuzi na ubunifu ili kuweza kujiajiri" amesema Lowassa.

Mkuu wa shule hiyo, Sista Anjali  Thomas amempongeza Lowassa kwa mchango alioutoa mpaka kikapatikana kiwanja cha ujenzi wa shule hiyo.