Lugola awaondoa madarakani maofisa wawili Nida

Muktasari:

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Kangi Lugola amewatengua madaraka maafisa wawili wa Mamlaka ya vitamburisho vya Taifa (Nida) mkoani Ruvuma kwa kosa kukaa  na namba za vitambulisho vya zaidi ya 14,000, bila kuwapelekea taarifa ili wananchi hao waweze kupata fursa ya kusajili laini zao  ambapo zoezi hilo linatarajia kukamilika Januari 20, 2020.

Songea. Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania, Kangi Lugola jana Alhamisi Januari 10, 2020 amewatengua madaraka maofisa wawili wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) wa mkoani Ruvuma kwa kosa la kutogawa namba za utambulisho wa Taifa (NIN).

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya soko kuu la Manispaa ya Songea mkoani humo, alisema  amewatengua vyeo maofisa wawili akiwemo ofisa wa Nida mkoa wa Ruvuma, Seifu Mgonja na ofisa wa Wilaya ya Tunduru.

Waziri Lugola aliyekuwa kwenye ziara ya siku moja mkoani humo alisema maofisa hao wamekuwa wakienda kinyume na maagizo ya Serikali la kuwataka waweze kuwakamilishia wananchi usajili wa laini za simu kwa alama za vidole kwa wakati.

 Akiyataja baadhi ya makosa kwa maofisa hao alisema ofisa wa mkoa  amekaa na namba za vitambulisho vya wananchi zaidi ya 14,000, bila kuwapelekea taarifa ili wananchi hao waweze kupata fursa ya kusajili laini zao  ambapo zoezi hilo linatarajia kukamilika Januari 20, 2020.

Kwa upande wa afisa wa Wilaya ya Tunduru ambaye hakumtaja jina  Waziri huyo alisema amekaidi wito wa kumtaka aweze kufika kwenye ziara yake ili wapeane taarifa pamoja na kuzitatua changamoto zinazowakabili katika zoezi hilo.

 “Siwezi kukubali upuuzi huu ni lazima watu tukipeana kazi tuzitekeleze kwa manufaa ya wananchi na Taifa, hivyo hao maafisa vyeo vyao nimevitengua kuanzia sasa.”

 “Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Pombe Maguli inawajali wanyonge hivyo mimi nikiwa Waziri wa Mambo ya Ndani nitapambana na watu wanaokwamisha jitihada za Serikali,” alisema Lugola.

Katika hatua nyingine Waziri huyo aliwataka askari polisi kufanya kazi zao kwa weledi, kwa kutenda haki pale wanapofanya kazi za wananchi hasa pale wanapohitaji huduma kwenye ofisi hizo.

 Alisema kumekuwepo na tabia ya askari kuwabambikizia kesi watu , kuwanyima dhamana bila sababu za msingi, kuwabambikia makosa wamiliki wa vyombo vya moto ambayo hata hayastahili kwa lengo la kujinufaisha.