MAUAJI YA LUMUMBA 1961: Lumumba afungwa gerezani mara mbili-2

Muktasari:

Maisha ya Patrice Lumumba yalijaa misukosuko. Si ajabu hata jina lake la asili lilikuwa ni Elias Okit’Asombo ambalo lilimaanisha ‘mrithi wa aliyelaaniwa,’ ambaye atakufa mapema.” Endelea…

Katika robo ya mwisho ya karne ya 19, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Italia na Ureno ziligawana bara la Afrika, lakini Mfalme Leopold II wa Ubelgiji ndiye aliyeichukua Jamhuri ya Congo na kuitawala.

Leopold II alikuwa mfalme wa Ubelgiji Desemba 10, 1865 hadi Desemba 17, 1909. Alimfuata baba yake Leopold I aliyekuwa mfalme wa kwanza baada ya kuanzishwa kwa taifa hilo.

Mwaka 1884, Marekani ililitambua “dola huru la Congo” chini ya mfalme huyo. Msingi wa yote haya uliwekwa katika Mkutano wa Berlin ulioanza Novemba 1884 kujadili kuigawa Afrika katika maeneo ya kiutawala. Ingawa aliitawala Congo na kufaidi utajiri wa rasilimali zake, Leopold hakuwahi kuikanyaga ardhi ya nchi hiyo.

Vuvumko la mataifa ya Kiafrika kujipatia uhuru lilianza katikati ya karne ya 20. Mwanadamu aliyekuja kuwa gumzo kubwa katika historia ya nchi hiyo ni Patrice Emery Lumumba aliyezaliwa Julai 2, 1925, wazazi wake wakiwa Francois Tolenga Otetshima (baba) na Julienne Wamato Lomendja.

Lumumba, aliyezaliwa katika familia ya Kikatoliki, ni wa kabila la Batelela. Alisoma shule za misheni na baada ya kufuzu masomo yake, alipata kazi ya ukarani wa posta.

Kazi hiyo ilimfanya ahame Kinshasa (wakati huo ikiitwa Leopoldville) kutokea Kasai. Baadaye alipanda cheo na kuhamishiwa posta ya Kisangani (wakati huo Kisangani ikijulikana kama Stanleyville). Maisha yake ya kisiasa yalianza 1955 alipoanza kushiriki harakati za kisiasa.

Jina lake halisi ni Elias Okit’ Asombo. Kwa mujibu Jonathan Reynolds katika kitabu chake, “30-Second Twentieth Century: The 50 Most Significant Ideas and Events, Each Explained in Half a Minute” (ukurasa wa 1885), maana ya jina hilo ni “mrithi wa aliyelaaniwa, ambaye atakufa mapema”.

“Baba yake alitaka (Lumumba) awe katekista,” anaandika Johannes Fabian katika kitabu chake cha “Remembering the Present: Painting and Popular History in Zaire”. Lakini baada ya kuelimika kiasi fulani, hakufuata njia hiyo aliyoitaka baba yake.

Alifukuzwa chuo cha kidini kwa sababu hakufuata sana mambo ya dini. Baadaye alijiunga na taasisi ya Kikatoliki ya Tshumbe-Sainte-Marie ambako pia alifukuzwa ndani ya mwaka. Baadaye alijiunga na Chuo cha Kimethodist cha utabibu, lakini huko pia alifukuzwa.

Baada ya hapo alirejea kijijini kwao na kufanya kazi yoyote aliyoipata huku akisoma karibu kila kitu alichokikuta katika maktaba ya Wembo-Nyama aliyokuwa akiitembelea mara kwa mara. Huko alikuwa akikutana na mwalimu wake wa awali, Joseph Logonya.

Baada ya kukaa kijijini muda mrefu, alihamia mjini na ndipo alipobadili jina, badala ya Elias Okit’Asombo, akaanza kuitwa Patrice Lumumba. Maisha yake mjini yalikuwa kati ya 1943 na 1956.

Lumumba alifanya kazi miezi minne katika kampuni ya kuchimba madini ya Symetian mjini Kalima jimbo la Maniema. Julai 1944 aliondoka na kwenda Kisangani.

Akiwa Kisangani alifanya kazi ya ukarani wa posta. Baada ya muda wa kazi alihudhuria masomo Marist Brothers ambayo ni moja ya shule za taasisi ya kidini ya Kikatoliki duniani.

Kwa kuvutiwa na utendaji kazi wake na bidii ya kusoma, wakubwa wake kazini walimpa cheo, kisha kumpeleka kituo cha kilimo cha Yangambi, karibu na mji wa Kisangani.

Mwaka 1947 alikubaliwa kujiunga na Chuo cha Posta cha Leopoldville. Kwa mujibu wa mwandishi Johannes Fabian, Lumumba alifaulu mitihani yake kwa kupata asilimia 94.4 na akapata ajira inayolingana na ya Wazungu waliokuwa wakifanya kazi Posta ya Congo.

Aliporudi Kisangani, akiwa ofisa mwandamizi wa posta, alikuwa akfanya mihadhara na kuandika. Alioa mwanamke kutoka kijiji alichozaliwa, lakini alikuwa na wanawake wawili awali; Mluba na mwingine Mcongo. Mwaka 1952 alikutana na kuanzisha urafiki na mwanasosholojia Mfaransa, Pierre Clement. Kwa mujibu wa kitabu “Lumumba: Africa’s Lost Leader” cha Leo Zeilig, Lumumba na Pierre walishirikiana kufanya tafiti za kijamii zilizomfumbua macho na kumfanya ajihusishe zaidi na harakati za kisiasa.

Mwaka 1954 alikutana na mwanasiasa wa Ubelgiji, Auguste Buisseret na kujiunga na jumuiya yao iliyokuwa Congo.

Katika kujihusisha na siasa, wanasiasa Ubelgiji walianza kuona changamoto kali kutoka kwake. Mawazo ya kuanza kumdhibiti yalianza baada ya ‘umachachari’ wake kuanza kuonekana bayana.

Julai 6, 1956 aliporejea kutoka Ubelgiji alikoalikwa na Buisseret kuzungumza katika jumuiya yao, alikamatwa mara aliposhuka kwenye ndege akituhumiwa kwa matumizi mabaya ya faranga 126,000 za Kifaransa za ofisi ya posta.

Alipopatikana na hatia alihukumiwa kifungo miaka miwili gerezani, lakini baadaye adhabu ilipunguzwa na kuwa miezi 18, lakini mwandishi Willame Jean-Claude katika kitabu chake, “Patrice Lumumba: The Congolese Crisis Revisited” anaamini kufungwa kwa Lumumba kulitokana na chuki na fitina za ajira zilizotengenezwa na Wazungu waliokuwa wakifanya kazi posta walipomwona anaelekea kuwazidi kitaaluma.

Umaarufu waongezeka

Kifungo hicho kilimfanya aanze kupata umaarufu zaidi hata nje ya Kisangani. Akiwa gerezani aliandika kitabu akidai Congo inahitaji ukombozi kamili.

Alitoka gerezani Juni 1958, akiwa tayari amepoteza kazi ya utawala katika Posta ya Congo. Kwa kuwa hakuwa na kazi nyingine Kisangani, aliamua kuhamia Kinshasa na kupata kazi ya usimamizi wa biashara katika kampuni ya bia ya Bas-Congo. Uvumi ukaibuka kuwa bia aina ya Polar inayotengenezwa na Bas-Congo ilikuwa ikiharibu nguvu za kiume. Alipambana na uvumi huo huku akijihusisha na siasa. Baadaye alijiunga na Joseph Ileo na Joseph Ngalula kuanzisha chama cha MNC (National Movement for Congo). Baada ya mwaka mmoja akawa kiongozi MNC. Agosti 1958 alichukua likizo na kwenda Brussels, Ubelgiji katika harakati za kisiasa.

Oktoba 5, 1958 alikiwakilisha chama hicho katika mkutano wa Waafrika uliofanyika Accra, Ghana. Kitendo cha kuhudhuria mkutano huo kilimfanya afahamike kwa wengi waliokuja kuwa viongozi wa nchi za Afrika baada ya uhuru.

Jumapili ya Januari 4, 1959 kulizuka ghasia za kisiasa katika Jimbo la Leopoldville. Ghasia hizo zilisababishwa na Waafrika waliotaka mabadiliko ya haraka. Walitaka uhuru bila kukawia. Vurugu zilizidi kusambaa maeneo mengine.

Vurugu hizo zilizuka katika mkutano wa hadhara wa MNC Oktoba 23, 1959 na kuchukua siku tano kutulia huku watu 30 wakiuawa.

Jumapili ya Novemba Mosi, Lumumba alikamatwa na serikali ya kikoloni na kuhukumiwa kifungo cha miezi sita gerezani. Tofauti na ilivyodhaniwa awali, kifungo hicho kiliongeza umaarufu wa Lumumba.

Itaendelea kesho…