MABADILIKO YA MSIMAMO: Profesa Kabudi anavyoshawishi

Monday December 2 2019

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi amekuwa gumzo nchini Kenya tangu wiki iliyopita baada ya kutoa hotuba iliyovuta hisia za wengi akiwaasa Wakenya dhidi ya siasa za ukabila.

Baadhi ya wadau wamesema hotuba hiyo imemuonyesha jinsi msomi huyo anavyoweza kubadilika kutokana na mazingira.

Baadhi ya wadau wamesema ni jambo la kawaida kwa viongozi kubadilika kutokana na mazingira na wakati.

Profesa Kabudi alizungumzia suala hilo wakati wa hafla ya uzinduzi wa ripoti ya Mpango wa Maridhiano wa Kenya (BBI) jijini Nairobi, Jumatano iliyopita.

Kabudi aliwachemsha viongozi wa Kenya wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo akisema kwamba wanafaa kuwaiga wenzao wa Tanzania kwa kupinga ukabila.

Katika hotuba yake, Profesa Kabudi alisema ijapokuwa Kenya ni taifa kubwa lenye watu wazuri, ukabila umekuwa ukiwarudisha nyuma na kuwataka wananchi kuwa na umoja na kufanya siasa za mshikamono na maendeleo badala ya siasa za kupigania mamlaka.

Advertisement

Aliwapongeza Rais Uhuru Kenyatta na waziri mkuu wa zamani wa nchi hiyo, Raila Odinga kwa kumaliza uhasama wao wa kisiasa baada ya uchaguzi wa 2017.

Hotuba hiyo ilipokelewa kwa bashasha na Wakenya katika mitandao ya kijamii.

“Speech (hotuba) ambayo hata muanzilishi wa urais Kenyatta hakuwahi toa, maongezi yenye busara na hekima nyingi,” ameandika mtu anayeitwa Hamis Maasai chini ya video ya hotuba hiyo iliyowekwa katika mtandao wa Youtube.

Naye Michael Egondi aliandika kwa Kiingereza chini ya video hiyo akisema “hii ni aina ya viongozi tunaowataka nchini Kenya si viongozi wanaoleta mambo hasi miongoni mwa Wakenya. Asante kwa hotuba nzuri”.

Ripoti ya BBI iliandaliwa baada ya Rais Kenyatta na Odinga kushikana mikono baada ya mvutano mkubwa baina yao uliotokana na uchaguzi mkuu wa mwaka 2017.

Viongozi hao waliamua kuja na mpango wa BBI, ambao unatoa dira ya namna ya kumaliza tofauti za kisiasa ambazo zimejijenga kwa misingi ya ukabila na umuhimu wa kuandaa uchaguzi huru na haki.

Ushawishi mkubwa na uwezo wa kujenga hoja ni vitu vinavyojitokeza haraka kila wakati Profesa Kabudi anapopata fursa ya kuzungumza.

Hata hivyo, tukio hilo linaonyesha jinsi Profesa Kabudi anavyotumia usomi wake kusoma mazingira na kujenga hoja kwa wakati uliopo.

Kabudi, ambaye anasifika kwa kuwa mjuzi wa lugha kutokana na kuzungumza Kiswahili fasaha na kutumia misamiati isiyo maarufu, wakati mwingine huonekana kuwa na misimamo tofauti katika jambo moja.

Kutokana na uwezo wake wa kuchambua mambo, Profesa Kabudi amekuwa mjumbe au kiongozi wa kamati au tume mbalimbali nchini.

Akiwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Profesa Kabudi alifanya kazi ya kuelimisha watu kuhusu umuhimu wa kumpunguzia Rais madaraka, akisema mengine hufanya yamtie doa na ndio maana walipendekeza awe na madaraka machache katika Muungano ambao ulitakiwa uwe na serikali tatu.

Lakini akiwa Waziri wa Sheria alisifu madaraka hayo ya Rais baada ya kuulizwa swali na mbunge, akisema katika masuala yote yanayohusu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mkuu wa nchi ni mmoja tu na ndiye amiri jeshi mkuu.

Akiwa mjumbe wa Tume ya Katiba alifanya kazi ya kuelimisha watu kuhusu umuhimu wa mabadiliko ya katiba kulingana na maoni ya watu yaliyowekwa kwenye Rasimu ya Katiba mwaka 2012.

Lakini miaka mitatu baadaye alipokuwa akijibu swali bungeni kama serikali ina mpango wowote wa kufanya marekebisho ya Katiba alisema hakuna umuhimu huo.

Profesa Kabudi alikuwa akijibu swali la Mbunge Juma Kombo Hamad (CUF), aliyetaka kujua kama Serikali ina mpango wa kubadili Katiba ili kuondoa kero za Muungano.

Profesa Kabudi alijibu hakuna mgongano mkubwa wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba ya Zanzibar unaosababisha ongezeko kubwa la kero za Muungano wala mgongano wa kimamlaka baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Alisema, kwa mujibu wa katiba zote mbili, itapotokea kuwapo kwa mgongano wa kikatiba tayari mamlaka zote mbili zimeelekezwa namna ya kutumia chombo maalumu kutatua kero hizo.

“Katiba imeweka utaratibu mahsusi katika mambo yanayobishaniwa na hadi sasa hakuna kero yoyote hata serikali iyapeleke huko, kwani imeweka utaratibu maalumu wa kutafsiri mgongano wowote haina sababu ya kupeleka mabadiliko ya Katiba,” alisema wakati huo.

Pia, Profesa Kabudi alisema Rais Magufuli ndiye mwenye mamlaka yote ya kuamua yanayohusu Tanzania kwani ndiye amiri jeshi mkuu na kiongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

Profesa Kabudi aling’ara nchini Kenya kutokana na jinsi alivyochambua kiini cha matatizo ya Wakenya na jinsi ya kuondokana nayo, akizinanga serikali nyingi za Afrika kwa kuweka nguvu ya kutawala na kusahau masuala mapana ya wananchi.

Tangu ameingia katika medani ya kisiasa kwa kuteuliwa kuongoza wizara tofauti--Sheria na Katiba na Mambo ya Nje-- amekuwa anatoa misimamo tofauti ya kisiasa, tofauti na aliyokuwa nayo wakati akiwa mhadhiri wa sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam au mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa chini ya Jaji Joseph Warioba.

Mara nyingi waziri huyo amekuwa akisema Tanzania ni nchi ya kidemokrasia na kutotoa misimamo yake pale inapotokea tofauti za kisiasa na amekuwa mkali kwa mashirika ya kimataifa na balozi ambazo zinataka kuingilia mambo ya ndani ya nchi.

Maoni ya wachambuzi

Baadhi ya watu wamechambua tabia ya baadhi ya viongozi kubadilika kutokana na mazingira.

Askofu wa Dayosisi ya Karagwe ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Benson Bagonza alisema anachokiona ni kwamba kuna tatizo mahali na kutaja makundi mawili ya wasomi.

“Baadhi ya wasomi wetu hivi sasa wamegawanyika katika makundi mawili. Moja ni wanaotawaliwa na hofu kuliko weledi au elimu yao...

“Viongozi wa dini huongozwa na dhamiri na msingi wa dhamiri ni neno la Mungu. Wasomi huongozwa na utafiti na uhuru wa taaluma yao,” alisema Askofu Bagonza.

Naye wakili wa kujitegemea wa Jijini Dar es Salaam, Frank Mushi alisema kubadilika ni tabia ya kibinadamu.

“Kubadilika ni tabia ya kibinadamu, sisi binadamu si wakamilifu na katika kutokuwa wakamilifu huwa tunabadilika hasa pale ambapo maslahi yetu yapo.

“Lakini pia mtu anayebadilika msimamo maana yake hakuwa na msimamo thabiti toka mwanzo, au hakuwa na msimamo kabisa bali alikuwa na maneno yanayoweza kupendeza hadhira yake,” alieleza Mushi.

Advertisement