Mageti CCM Kirumba yafungwa, TV kubwa zafungwa Furahisha

Muktasari:

  • Mageti na milango yote ya kuingilia uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza nchini Tanzania yanakofanyika maadhimisho ya kitaifa ya miaka 58 ya Uhuru wa Tanganyika yamefungwa baada ya wananchi kufurika tangu saa 10:00 alfajiri.

Mwanza. Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza nchini Tanzania umefurika! Milango na mageti yote yamefungwa kuzuiwa watu kuingia.

Badala yake, wote waliosalia kwenye misururu mirefu ya kuingia uwanjani wameelekezwa kwenda uwanja jirani wa Furahisha.

Ili kuwawezesha wananchi hao kushuhudia kinachoendelea, runinga kadhaa zimefungwa uwanjani wa Furahisha ambako kila anayefika huelekezwa eneo la kuketi na kutakiwa kutulia.

Kutoka uwanja wa CCM Kirumba yanakofanyika maadhimisho ya Kitaifa ya miaka 58 ya Uhuru wa Tanganyika leo Jumatatu Desemba 9, 2019 hadi uwanja wa Furahisha ni umbali wa hatua zisizozidi 300.

Wingi wa watu walioko uwanja wa Furahisha ni zaidi ya wale waliofanikiwa kuingia uwanjani.

“Mimi niko hapa uwanjani tangu saa 12:00 asubuhi lakini nimeshindwa kuingia kutokana na msururu wa watu niliowakuta mlangoni wakitaka kuingia uwanjani,” anasema Hassan Ramadhani, mkazi wa Kilimahewa jijini Mwanza

Ndivyo mtu anaweza kusema kuzungumzia hamasa ya wakazi wa jiji na mkoa wa Mwanza na vitongoji vyake walivyojitokeza kuhudhuria maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru wa Tanganyika yanayoadhimishwa Kitaifa jijini humo.

Mkuu wa mkoa wa Mwanza, John Mongella amesema wingi wa watu umetokana na mapenzi ya Watanzania kwa Serikali na Taifa lao, hamasa na ushirikishwaji wa kila kada ya uongozi uliofanywa na kamati ya maandalizi.

“Tumetoa hamasa kupitia matangazo kwa njia mbalimbali kuanzia vyombo rasmi vya habari, mitandao ya kijamii, magari ya matangazo ya magari mitaani pamoja na viongozi wa Serikali za mitaa,” amesema Mongella

Milango ya kuingilia uwanja wa CCM Kirumba ilifunguliwa tangu saa 10:00 alfajiri ya leo Jumatatu Desemba 9, 2019 ambapo kufikia saa 1:30, majukwaa yote ya uwanja huo wenye uwezo wa kuingiza zaidi ya watu 25, 000 yalikuwa yamejaa.