Magufuli: Makamba, Ngeleja waliniomba radhi, nimewasamehe

Muktasari:

Rais John Magufuli wa Tanzania amesema wabunge wa CCM, January Makamba na Willium Ngeleja walikwenda kumwomba msamaha kutokana na kuhusika kwao kwenye sauti zilizokuwa zikielezea mipango mbalimbali ndani ya CCM na Serikali.


Dar es Salaam. Unazikumbuka zile sauti  za vigogo wa Serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM) zilizokuwa zinasambaa mitandaoni? Kama unakumbuka basi sikia hii.

Leo Jumatano Septemba 4,2019 Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema miongoni mwa waliohusika katika hizo sauti ni wabunge wa CCM, January Makamba (Bumbuli) na William Ngeleja (Sengerema), walimwomba msamaha.

Akizungumza leo na wataalamu wa ujenzi nchini, Rais Magufuli amesema sauti hizo kwa zaidi ya asilimia 100  zilikuwa za kweli na alipofikilia kama suala hilo litakwenda katika kamati ya maadili ya CCM  hali ingekuwa mbaya kwao.

Kiongozi huyo alieleza umuhimu wa kusamehe pale mtu anapokukosea na kuwaeleza wataalamu hao kwamba amewasamehe waliomkosea.

Baada ya kueleza kwa ufupi kuhusu sauti hizo, Rais Magufuli akasita kidogo kuendelea kuzungumza kisha akacheka, “nikasema hawa wakipeleka katika kamati ya maadili (ya CCM) adhabu itakuwa kubwa.”

“Lakini wakajitokeza wawili wakaniomba msamaha, nikawa najiuliza mimi kila siku naomba msamaha kwa Mungu na ile sala tusamehe makosa yetu kama tunavyowasamehe.”

Aliongeza, “Hawa waliokuja kuniomba msamaha mheshimiwa Makamba na Ngeleja niliamua kuwasamehe. Waliomba msamaha, wakanigusa, nikasamehe na kusahau.”

“Kwa hiyo suala la kusamehe ni muhimu, hata akikuudhi, akikutukana namna gani na hata akifanya kazi vibaya akaja kukuomba msamaha namna gani.”

Rais Magufuli alikuwa anazungumza katika mkutano wa siku mbili ulioanza leo Dar es Salaam unaohusisha Bodi ya usajili wa Makandarasi (CRB), Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB),  Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB).