VIDEO: Magufuli asifu demokrasia ndani ya CCM

VIDEO: Magufuli asifu demokrasia ndani ya CCM

Muktasari:

Mgombea Urais wa CCM, John Magufuli amesema Chama chake kinafuata misingi ya demokrasia katika utendaji ndiyo maana waliamua kumpitisha Mohammed Moni kugombea jimbo la Chemba badala ya Juma Nkamia

Dar es Salaam.  Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama cha Mapinduzi (CCM), John Magufuli amesema chama chake kinafuata misingi ya demokrasia katika utendaji, ndiyo maana waliamua kumpitisha Mohammed Moni kugombea jimbo la Chemba badala ya Juma Nkamia.

Amesema uamuzi huo ulifikiwa baada ya kuona wananchi wa Chemba wanamhitaji Mohammed kwa kumpitisha katika kura na maoni na kumshinda Nkamia aliyekuwa mbunge wao.

Magufuli aliyasema hayo katika mkutano wake alioufanya wilaya ya Chemba akiwa njiani kuelekea Dodoma ambapo pia aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo Juma Nkamia alipata nafasi ya kumuombea kura.

“Mimi ndiyo mwenyekiti wa kamati kuu, mimi ndiye mwenyekiti wa NEC, nilifahamu kuwa kuna Mohammed Moni ambaye ameongoza kura na mwanafunzi wangu (Juma Nkamia) aliyefuatia,”

“Chama cha mapinduzi kinafuata demokrasia, ingekuwa hivi ningemteua mwanafunzi wangu kwa sababu nilimfundisha aje agombee hapa lakini uamuzi wa watu wa Chemba na CCM walimtaka Mohammed ndiyo maana nimemleta,” amesema Magufuli.

Amesema kwa wengine waliogombea kazi zipo nyingi, huku akibainisha kazi za kuchaguliwa ni za kuachiana.

“Mlitaka Nkamia akae hapa miaka mingapi, Nyerere (Rais wa kwanza wa Tanzania – Julius) alikaa miaka mingi akang’atuka mwenyewe, akaja Mzee Mwinyi (Rais wa awamu ya pili - Ali Hassan) akakaa miaka 10 akapumzika,”

“Akaja Mzee Benjamini Mkapa (Hayati-Rais wa awamu ya tatu) miaka 10 akapumzika, akaja Rais wa awamu ya nne Jakaya Kikwete akakaa miaka 10 akapumzika, mimi nimekaa mitano mnataka mnipumzishe, mtanipa mitano mingine nikae kama wenzangu,” alihoji Magufuli.

Alitumia nafasi hiyo pia kuahidi kushughulikia changamoto mbalimbali ikiwamo ujenzi wa stendi ya kisasa, kupeleka umeme vijiji 50, kukamilisha ujenzi wa kituo cha polisi wilaya, shule ya sekondari katika eneo la makao makuu ya wilaya na upungufu wa vyumba vya madarasa katika shule za msingi.