Magufuli awataka watendaji kata kuwawajibisha mawaziri, wakurugenzi na ma-RC
Muktasari:
Rais wa Tanzania, John Magufuli amewataka watendaji wa kata nchini kutoa taarifa kuhusu wakurugenzi, mawaziri na wakuu wa mikoa wanaofanya matendo yanayokiuka misingi ya utawala bora.
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amewataka watendaji wa kata nchini kutoa taarifa kuhusu wakurugenzi, mawaziri na wakuu wa mikoa wanaofanya matendo yanayokiuka misingi ya utawala bora.
Ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Septemba 2, 2019 Ikulu jijini Dar es Salaam alipokutana na watendaji hao kutoka mikoa yote nchini.
Amebainisha kuwa mtendaji wa kata ndio bosi wa eneo lake, “Hata kama kuna kiongozi wa nafasi gani yuko chini yako na anapoonekana kuenenda visivyo unapaswa kumwajibisha au kutoa taarifa kwa mamlaka yake.”
“Katika kata kuna mkurugenzi wa halmashauri, RC (mkuu wa Mkoa), waziri au nani, wewe (mtendaji kata) ndio msimamizi, kama wewe upo katika kata na ambayo kuna waziri, RC, mkurugenzi sijui nani wewe ndiyo msimamizi,” amesema Magufuli.
Ameongeza, “Usiogope kumlima (barua) na kumwandikia maoni, hata kama anakuzidi cheo kwamba katika kata hii namwona mtumishi huyu anakwenda kinyume na maadili. Na ukimwona ni mkubwa sana, piga nakala hapa kwangu, lazima watu tujifunze kuogopana.”
Huku akizungumza zaidi kwa mifano amesema, “Kila siku anapigana (kiongozi) baa katika kata yako kwa sababu ni mkubwa unaacha kumripoti, chalaza kalamu na ndio maana watendaji kata wana kalamu na saini zao.”
Huku akiwataka kutokubali kudharaulika katika maeneo yao, Magufuli amesema, “Hapa (Ikulu) ni kwenu na mimi ni mpangaji tu hapa na mnaoamua nani aende Ikulu ni nyinyi na wananchi.”
“Hapa wamekaa hadi Wajerumani, amekaa Nyerere (Julius) akaondoka, akaja Mwinyi (Ali Hassan) akaondoka, amekuja Mkapa (Benjamin) akaondoka, amekuja Kikwete (Jakaya) akaondoka na mimi nitakaa na kuondoka,” amesema.
“Ndio maana sikusita kuwakaribisha , najua mko mahali pema salama na nilifikiri ni eneo hili tu tunaweza kukaa na kuzungumza vizuri. Nikija wilayani hawawasogezi karibu,” amesema.