Mahakama Tanzania kutoa maelekezo TLS kujiunga kesi ya urais

Muktasari:

  • Kesi ya mkulima ya Patrick Dezydelius Mgoya anayehoji ukomo wa kugombea urais wa Tanzania imeendelea kushika kasi ambapo Mahakama Kuu ya Tanzania itatoa maelekezo muhimu uamuzi kuhusu maombi ya Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kuomba kuunganishwa kwenye kesi hiyo.

Dar es Salaam. Mahakama Kuu ya Tanzania imepanga kutoa maelekezo muhimu kuhusu maombi ya Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kujitosa katika kesi ya kikatiba inayohusu ukomo wa urais nchini humo, iliyofunguliwa na Mkulima, Patrick Dezydelius Mgoya.

TLS kimefungua maombi Mahakama Kuu kikiomba kuunganishwa katika kesi hiyo, huku katika hati ya faragha ya maombi hayo kikieleza kuwa kinaomba kuunganishwa katika shauri hilo kama mdaiwa mwenyewe maslahi.

Maombi hayo yaliyosajiliwa rasmi mahakamani Novemba 5, 2019, yalitajwa kwa mara ya kwanza jana Jumatatu Novemba 11, 2019 huku Mgoya ambaye ni mjibu maombi wa kwanza ndiye pekee aliyefika mahakamani.

Mjibu maombi wa pili, Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa niaba ya Serikali hakuwepo mahakamani wala mwakilishi wake, jambo ambalo lilimfanya Jaji Benhajj Masoud anayesikiliza maombi hayo ahoji kama alipewa taarifa na nyaraka za maombi hayo.

Wakili wa TLS, Suzan Kawanga aliieleza mahakama kuwa walimpa taarifa na nyaraka za maombi hao, tangu Ijumaa iliyopita, Novemba 8, mwaka huu.

Baada ya majadiliano mafupi kati yake na Mkulima Mgoya, Jaji Masoud alimpa siku tatu kuwasilisha kiapo kinzani kama atakuwa na hoja za kupinga maombi hayo kabla au kesho Jumatano.

Pia, Jaji Masoud alipanga maombi hayo yatajwe keshokutwa Alhamisi Novemba 14, 2019 kwa ajili ya kutoa maelekezo muhimu na akamwagiza wakili wa TLS, kumjulisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ili afike mahakamani siku hiyo.

TLS katika kiapo cha Makamu wake wa  Rais, wakili Mpale Mpoki, kinaeleza kuwa miongoni mwa majukumu ya taasisi hiyo ni kulinda na kuisaidia jamii katika masuala yote ya kisheria na kuisaidia Serikali na mahakama masuala yote yanayoathiri utungwaji na usimamizi wa sheria nchini.

Wakili Mpoki anaeleza shauri hilo lililofunguliwa na Mkulima lina maslahi kwa umma hivyo matokeo yake yanaweza kuwa ana athari kwa umma nzima na kwamba mwombaji (TLS) ataathirika na matokeo hayo ya shauri hilo lililotajwa.

Wakili Mpoki, anasisitiza katika kiapo hicho kuwa kama TLS hakitaunganishwa katika shauri hilo kitakuwa kimenyimwa haki ya kusikilizwa ambayo ni haki ya msingi.

Mgoya, maarufu kama Mkulima amefungua kesi hiyo Mahakama Kuu, Masjala Kuu dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, akiiomba itoe tafsiri ya maana sahihi na athari za masharti ya Ibara ya 40(2) ya Katiba ya Nchi inayoweka ukomo wa mtu kuchaguliwa kuwa rais.

Anadai kuwa masharti ya ibara hiyo ya 40(2) ya mihula miwili tu ya raia kuchaguliwa kuwa rais yaani miaka 10 tu yanakiuka haki za kikatiba za Ibara za 13, 21 na 22(2) hasa kushiriki katika shughuli za utawala kwa kuchagua na kuchaguliwa.

Hata hivyo, Serikali kupitia kwa AG tayari imeshamwekea pingamizi la awali ikiiomba mahakama hiyo iitupilie mbali pamoja na mambo mengine ikidai kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo, na kwamba kesi hiyo ina kasoro za kisheria ambazo haziwezi kurekebishika.

Pia, Serikali inadai kuwa mwombaji hana haki ya kisheria kufungua na kwamba nafuu anazoziomba mwombaji haziwezi kutolewa kwa kuwa zinakiuka kifungu cha 44 cha Sheria ya Mawakili, Sura ya 341, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Shauri la msingi linalosikilizwa na jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Kiongozi Dk. Eliezer Feleshi, akishirikiana na Jaji Dk. Benhajj Masoudu na Jaji Seif Kulita, limepangwa kutajwa Novemba 22, 2019, kwa ajili ya maelekezo muhimu.