Mahakama Tanzania yataka vithibitisho kuumwa James Rugemarila

Thursday January 16 2020

 

By Pamela Chilongola, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam nchini Tanzania imemuamuru tarehe ijayo ya kesi ya Mkurugenzi wa VIP na mmiliki mwenza wa zamani wa IPTL, James Rugemarila kufika na vithibitisho vya hospitali.

Hatua hiyo imekuja baada ya hakimu Mkazi Mwandamizi, Vicky Mwaikambo kutaka kujua sababu ya kutofika mshtakiwa huyo mahakamani ndipo mmoja wa askari magereza kudai Rugemarila ni mgonjwa.

Leo Alhamisi Janauri 17, 2020 Hakimu Mwaikambo amesema wamepokea taarifa ya kuumwa kwa Rugemarila hivyo shauri hilo litakapokuja tarehe ijayo mshtakiwa huyo ahakikishe anapeleka vithibitisho vya hospitali.

Awali, wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Godliver Kiriani amedai shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake bado unaendelea.

Shauri hilo limeahirishwa hadi Januari 30, 2020 litakapokuja kwa ajili ya kutajwa.

Mbali na Rugemarila wengine ni Harbinder Seth ambaye alikuwa Mwenyekiti Mtendaji wa PAP na Mwanasheria wa kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), Joseph Makandege.

Advertisement

Miongoni mwa mashtaka 12 yanayowakabili ni ya uhujumu uchumi mashtaka matano ya kutakatisha fedha na kuisababisha hasara ya USD 22, 198,544.60 na Sh309.46 bilioni.

Mashtaka hayo yanayowakabili ni pamoja na kula njama, kujihusisha mtandao wa uhalifu, kughushi nyaraka, kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kuisababishia Serikali hasara na kutakatisha fedha.

Miongoni mwa mashtaka hayo ni kudaiwa, kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19, 2014 jijini Dar es Salaam, Rugemarila na Sethi walikula njama katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Washtakiwa wote, wanadaiwa kati ya Novemba 28/29, 2011 na Januari 23,2014 makao makuu Benki ya Stanbic kinondoni na Benki ya Mkombozi tawi la St .Joseph kwa ulaghai washtakiwa hao walijipatia kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), walijipatia USD 22,198,544.60 na Sh309.461 bilioni.

 

Advertisement