VIDEO: Mahakama yaelezwa Erick Kabendera hapumui vizuri

Muktasari:

Kesi inayomkabili mwandishi wa habari nchini Tanzania, Erick Kabendera iliitwa kwa ajili ya kutajwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam ambapo upande wa mashtaka umeileleza mahakama hiyo kuwa upelelezi bado haujakamilika huku mawakili wa utetezi ukidai mteja wao anaumwa hivyo anahitaji kupatiwa matibabu.

Dar es Salaam. Upande wa utetezi katika kesi inayomkabili mwandishi wa habari nchini Tanzania, Erick Kabendera umeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kuwa mteja wao bado anaumwa mguu wa kulia, hatembei vizuri na ana shida ya kupumua.

Kabendera, mwandishi wa habari za ndani na nje ya Tanzania alifikishwa  Mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Agosti 5, 2019 akikabiliwa na mashtaka matatu, ambayo ni kuongoza genge la uhalifu, kukwepa kodi na kutakatisha zaidi ya Sh173.2 Milioni

Leo Alhamisi Septemba 12,2019, wakili  wa utetezi, Jebra Kambole amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Agustine Rwizile baada ya Wakili Mwandamizi wa Serikali Wankyo Saimon kueleza upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

“Mteja wetu ni mgonjwa mpaka sasa anashindwa kutembea vizuri mguu wa kulia umepooza na anashindwa kupumua vizuri hasa usiku.”

"Mteja wetu angepata vipimo vizuri, tunaiomba Mahakama kuielekeza idara ya magereza wampe fursa ya kupatiwa matibabu hospitali yoyote ya serikali na sisi mawakili tujue anaumwa nini," amedai  Wakili Kambole

Hata hivyo, wakili Wakyo ameieleza magereza wana utaritibu wao hasa panapokuwa na mgonjwa na mara ya mwisho walifuatilia kujua kama amepatiwa matibabu na mkuu wa gereza  alimuhakikishia kuwa anatibiwa.

Mwananchi  lililokuwepo mahakamani, limemshuhudia Kabendera ambaye wakati akitoka na kuingia mahakamani hapo alikuwa akitembea kwa shida tofauti na siku nyingine.

Hakimu Rwizile baada ya kusikiliza hoja za upande zote ameahirisha kesi hiyo hadi Septemba 18, 2019 itakapotajwa tena na kuangalia huduma ambayo atakuwa  ameipata.

 

Katika kesi ya msingi,  mshtakiwa anadaiwa katika siku tofauti tofauti kati ya Januari 2015 na Julai 2019 katika maeneo tofauti jijini Dar es Salaam, mshtakiwa Kabendera alitoa msaada katika genge la uhalifu kwa nia ya kujipatia faida.

Katika shtaka la pili, lililosomwa na Wakili Wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi imedaiwa, siku na mahali hapo mshtakiwa bila kuwa na sababu za msingi kisheria alishindwa kulipa kodi ya Sh173.24 milioni ambayo ilitakiwa ilipwe kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Katika shtaka la utakatishaji fedha lililosomwa na Wankyo Simon imedaiwa kati ya Januari 2015 na Julai 2019 ndani ya jiji na mkoa wa Dar es Salaam mshtakiwa alijipatia kiasi hicho cha Sh173.24 milioni wakati akizipokea alijua kuwa fedha hizo ni mazao ya makosa tangulizi ya kukwepa Kodi na kujihusisha na genge la uhalifu.

Hata hivyo, mshtakiwa Kabendera hakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo isipokuwa kwa kupata kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP)