Mahakama yatoa amri wabunge wanne Chadema kukamatwa

Muktasari:

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Ijumaa Novemba 15, 2019 imeamuru wabunge wanne wa Chadema kukamatwa kwa kukiuka masharti ya dhamana.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Ijumaa Novemba 15, 2019 imeamuru wabunge wanne wa Chadema kukamatwa kwa kukiuka masharti ya dhamana.

Wabunge hao na majimbo yao kwenye mabano ni John Heche (Tarime Vijijini), Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini), Halima Mdee (Kawe) na Ester Bulaya (Bunda).

Amri hiyo imetolewa leo na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba baada ya wabunge hao kutokuwepo mahakamani bila taarifa yoyote. Hata wadhamini wao pia hawakuwepo.

Pia, Hakimu Simba ametoa hati ya wito wa wadhamini wa wabunge hao kujua sababu za kutowapeleka washtakiwa mahakamani.

Kabla ya kutoa amri hizo, Hakimu Simba amesema leo kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa, washtakiwa wengine waliwahi lakini wabunge hao wanne hadi saa 4:05 asubuhi walikuwa hawajafika mahakamani bila sababu za msingi.

Baada ya Hakimu Simba kueleza hayo wakili wa upande wa utetezi, Faraji Mangula aliyewawakilisha mawakili Profesa Abdallah Safari, Peter Kibatala na Jeremiah Mtobesya ameieleza mahakama hiyo kuwa ana taarifa za Bulaya.

Kauli ya Mangula ilipingwa na Hakimu Simba aliyebainisha kuwa anayepaswa kuzungumza kuhusu washtakiwa kutofika mahakamani ni wadhamini si wakili.

Kwa pamoja wanakabiliwa na  mashtaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia na kuhamasisha hisia za chuki.

Pia, wanadaiwa kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi wa makosa yanayodaiwa kutendeka kati ya Februari 1 na 16, 2018, jijini Dar es Salaam.

Mbali na wabunge hao wanne, wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe; mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko; katibu mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji na naibu makatibu wakuu, Salum Mwalimu (Zanzibar) na John Mnyika (Bara).