Takukuru yabaini dosari utekelezaji miradi ya maendeleo Tanga
Muktasari:
- Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Tanga imechukua hatua mbalimbali baada ya kubaini dosari kadha katika matumizi ya fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Tanga. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Tanga imebaini dosari mbalimbali katika usimamizi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hali inayohatarisha matumizi sahihi ya fedha za umma na thamani halisi ya uwekezaji wa Serikali.
Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Tanga, Ramdhani Ndwatah amesema pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, bado kuna changamoto za udhaifu wa usimamizi kwa baadhi ya wadau wenye dhamana ya kusimamia miradi hiyo.
Ndwatah ametoa kauli hiyo leo, Julai 22, 2026 wakati wa warsha ya wadau wa usimamizi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo, iliyoandaliwa na Takukuru jijini Tanga. Warsha hiyo ilmefunguliwa na Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Salim Nyamwese, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Batilda Burian.
Amesema ufuatiliaji wa matumizi ya rasilimali za umma unaofanywa na Takukuru umebaini dosari mbalimbali, zikiwemo viashiria vya uvujaji wa rasilimali, ucheleweshaji wa utekelezaji wa miradi, ushiriki mdogo wa wadau na hatari ya kutopatikana kwa thamani halisi ya fedha zilizowekezwa.
"Kutokana na dosari hizo, Takukuru imeendelea kuchukua hatua kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329, Marejeo ya mwaka 2023," amesema Ndwatah.
Ameongeza kuwa taasisi hiyo inatarajia warsha hiyo itasaidia kuimarisha mfumo wa usimamizi wa fedha za miradi ya maendeleo pamoja na kuongeza uwajibikaji wa wadau wote wanaoshiriki katika utekelezaji wa miradi hiyo.
"Tunatarajia baada ya warsha hii kutakuwa na usimamizi wa karibu zaidi wa fedha za miradi ya maendeleo na kuongezeka kwa uwajibikaji wa wadau ili kuhakikisha malengo yaliyokusudiwa yanafikiwa," amesema.
Kwa upande wake Nyamwese, amewataka wakurugenzi wa halmashauri na wasimamizi wa miradi katika Mkoa wa Tanga kuhakikisha wanasimamia ipasavyo utekelezaji wa miradi ili fedha zinazotolewa na Serikali ziwanufaishe wananchi.
Amesema Serikali imeendelea kupeleka fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali, ikiwemo elimu, afya, maji, miundombinu na uwezeshaji wa uchumi wa wananchi, hivyo haitavumilia uzembe unaoweza kukwamisha utekelezaji wa miradi hiyo.
"Serikali haitavumilia kuona usimamizi usioridhisha unaharibu mipango ya maendeleo," alisema Nyamwese.
Baadhi ya wadau wa maendeleo, wakiwemo wawakilishi wa asasi za kiraia zinazoshiriki katika ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za umma (PETS), wameipongeza Takukuru kwa kuweka wazi dosari zilizobainika na kutaka hatua kali zichukuliwe dhidi ya watakaobainika kuhujumu miradi ya maendeleo.
Mtaalamu wa masuala ya fedha, Ramdhani Manyeko, amesema hatua za kisheria zinapaswa kuendelea kuchukuliwa dhidi ya wote watakaobainika kuhusika na ubadhirifu wa fedha za umma.
"Takukuru imeonyesha utayari kwa kuchunguza na kubaini dosari katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Tunatarajia wale watakaobainika kuhusika na ubadhirifu wawajibishwe kwa mujibu wa sheria ili kulinda rasilimali za umma," amesema Manyeko.