Takukuru yakabidhiwa rungu miradi ya maendeleo Iringa
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Elia Luvanda, akizungumza na washiriki wa kikao cha wadau wa usimamizi wa programu na miradi ya maendeleo mkoani Iringa, kilichoandaliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo.
Muktasari:
- Takukuru imeeleza kuwa warsha ya wadau wa usimamizi wa utekelezaji wa programu na miradi ya maendeleo mkoani Iringa inalenga kuwajengea uwezo viongozi na wataalamu kuhusu usimamizi bora wa miradi, kuimarisha uwajibikaji, kuzuia mianya ya rushwa na kuhakikisha miradi ya maendeleo inakamilika kwa wakati, kwa ubora unaotakiwa na kutoa huduma zilizokusudiwa kwa wananchi.
Iringa. Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James ameipa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani humo jukumu la kuchukua hatua dhidi ya wasimamizi wa miradi ya maendeleo watakaoshindwa kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa wakati, ubora na thamani ya fedha inayotakiwa.
RC James amesema Serikali imeendelea kuwekeza fedha nyingi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, lakini bado baadhi ya miradi imekuwa ikikabiliwa na changamoto za ucheleweshaji, ubora usioridhisha na mingine kukamilika bila kutoa huduma zilizokusudiwa.
Akizungumza Juni 24, 2026, katika kikao cha wadau wa usimamizi wa programu na miradi ya maendeleo mkoani Iringa, kilichoandaliwa na Takukuru katika ukumbi wa Ofisi ya Mkoa, RC James amesema ipo haja ya kuwajengea uwezo viongozi na wataalamu wanaosimamia miradi ili kuondoa dosari zinazojitokeza wakati wa utekelezaji.
“Bado kuna changamoto katika manunuzi, usimamizi na ufuatiliaji wa miradi. Ni muhimu viongozi na wataalamu wafahamu sheria, kanuni na taratibu za usimamizi wa miradi ili kuepuka kasoro zinazoweza kujitokeza,” amesema RC James.
RC James amesema baada ya mafunzo hayo hakuna sababu ya kuendelea kushuhudia miradi yenye dosari, akisisitiza kuwa Takukuru inapaswa kuchukua hatua kwa watakaobainika kushindwa kutekeleza wajibu wao.
“Baada ya maelezo haya, mradi ukianza usiniambie mnachunguza, muelekeze moja kwa moja nani anahusika na hatua zichukuliwe,” amesema RC James.
Aidha, RC James alitaja baadhi ya miradi mikubwa inayotekelezwa mkoani Iringa kuwa ni pamoja na miradi ya Iruwasa yenye thamani ya zaidi ya Sh200 bilioni, Ruwasa zaidi ya Sh64 bilioni, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Sh18 bilioni na mradi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (Muce) wenye thamani ya zaidi ya Sh120 bilioni.
“Na dhamira ya Serikali ni kuona miradi hiyo inakamilika kwa wakati, inatoa huduma zilizokusudiwa na wananchi wanashuhudia matokeo ya fedha zinazotolewa,” amesema RC James na kuongeza kuwa baadhi ya fedha za miradi zimekuwa zikirejeshwa Serikalini baada ya kushindwa kutumika ndani ya mwaka wa fedha kutokana na ucheleweshaji wa utekelezaji.
“Sasa tunaona fedha zinafika lakini miradi haitekelezwi hadi mwaka wa fedha unaisha na fedha zinarudi, na hii inaweza kuashiria mtu anatafuta mkandarasi au mzabuni anayemtaka, na naiomba Takukuru kufanya uchunguzi wa kina,” amesema.
Akizungumza katika warsha hiyo, Ofisa wa Takukuru Mkoa wa Iringa, Evarist Shija, amesema taasisi hiyo imeendelea kutoa elimu kwa wadau wa maendeleo ili kuimarisha usimamizi wa programu na miradi ya maendeleo.
Shija amesema uchunguzi na ufuatiliaji uliofanywa mwaka 2023 ulionyesha kuwa miradi 18 kati ya miradi 364 iliyofuatiliwa ilikuwa na changamoto mbalimbali zilizohitaji hatua za maboresho.
Kwa mujibu wa Shija, baadhi ya changamoto zilizobainika ni kuanzishwa kwa miradi bila uwepo wa fedha za kutosha, usanifu usiojitosheleza na udhaifu katika usimamizi wa utekelezaji.
Shija ametolea mfano mradi wa maji wa Ihemi-Ifunda ambao umechelewa kukamilika kutokana na changamoto mbalimbali za utekelezaji.
Naye Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa, Elia Luvanda, amesema mafunzo hayo yamefanyika wakati muafaka kutokana na kuwa ni mwisho wa mwaka wa fedha 2025/2026 na yataisaidia mkoa kuingia katika mwaka wa fedha 2026/2027 ukiwa na msingi mzuri wa usimamizi wa miradi.
“Iringa imara tutaijenga kwa umoja na uwajibikaji, na Takukuru wameona umuhimu wa kuweka misingi imara ya usimamizi wa miradi ya maendeleo,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga, Fidelica Myovela, amesema viongozi wanapaswa kusimamia matumizi ya fedha za miradi kuanzia ngazi za chini hadi juu ili kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana kupitia matokeo ya miradi inayotekelezwa.
Naye Ofisa Mipango kutoka Wilaya ya Mufindi, Peter Ngussa, ameshauri mafundi wa maeneo husika washirikishwe katika utekelezaji wa miradi ili kupunguza gharama na kuongeza ufanisi, huku akisisitiza kuwa miradi inapaswa kujengwa katika maeneo yenye mahitaji halisi ya wananchi ili kuleta tija iliyokusudiwa.