Majaliwa: Uzalishaji mbegu za michikichi unaridhish

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa

Muktasari:

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema ameridhishwa na hatua iliyofikiwa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari) katika uzalishaji wa mbegu bora za zao la michikichiki katika kituo cha taasisi hiyo mkoani Kigoma.

Kigoma. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema ameridhishwa na hatua iliyofikiwa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari) katika uzalishaji wa mbegu bora za zao la michikichiki katika kituo cha taasisi hiyo mkoani Kigoma.

Alieleza hayo jana Ijumaa Februari 21, 2020 alipotembelea kituo cha utafiti wa zao la michikichi cha Tari Kihinga kilichopo wilayani Kigoma alipokuwa katika ziara yake ya siku moja mkoani Kigoma.

Akiwa kituoni hapo, Waziri Mkuu alipokea taarifa ya utafiti juu ya uendelezaji wa zao la michikichi uliofanywa na Tari kuanzia mwaka 2018, ambapo hadi kufikia Februari 15, 2020 taasisi hiyo ilikuwa imezalisha mbegu 1,525,017 ambazo zinaweza kupandwa katika shamba lenye ukubwa wa ekari 30,500.

Waziri Mkuu amesema Serikali imeamua kulipa kipaumbele zao la michikichi kwa lengo la kumaliza tatizo la upatikanaji wa mafuta ya kula nchini, hivyo ufufuaji zao hilo utaliwezesha Taifa kuzalisha mafuta ya kutosha kwa ajili ya mahitaji ya ndani na ziada itakayobakia itauzwa nje ya nchi.

Kufuatia hatua hiyo, amewataka wananchi hasa vijana kuchangamkia fursa ya kulima zao hilo kwa wingi kwa kuwa upo uhakika wa kupata mbegu bora na pia zao hilo litawakwamua kiuchumi na kuwaondolea umasikini wa kipato.

Pia, amewaagiza maofisa ugani kuwafuata wakulima katika maeneo yao na kuwaelekeza namna ya kulima zao hilo kuanzia hatua za awali za utayarishaji mashamba, matumizi bora ya pembejeo ili waweze kulima kisasa na kujiongezea tija.

Baada kutembelea kituo hicho, alizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Mwanga Community Centre uliopo manispaa ya Kigoma Ujiji, ambapo pamoja na mambo mengine aliwataka watumishi wa umma watenge muda ya kusikiliza kero za wananchi.

“Watumishi mnatakiwa kwenda kwa wananchi na kusikiliza kero zinazowakabili na kushirikiana nao katika kuzipatia ufumbuzi..., hamuendi na kama mngekuwa mnaenda kusingekuwepo na mabango kwani kitendo cha kuwepo mabango ni ishara tosha kwamba hamuendi,” amesema.

Majaliwa Serikali imepeleka fedha nyingi mkoani Kigoma  kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo zikiwemo Sh 4.6 bilioni kwa ajili ya ununuzi wa dawa, ambapo Manispaa ya Kigoma Ujiji inapata Sh50 milioni kila mwezi hivyo hakuna sababu ya wananchi kukosa dawa.

Amesema Serikali imedhamiria kuboresha na kusogeza huduma za afya kwa kujenga vituo vya afya karibu na makazi ya wananchi zikiwemo za afya ili kuwapunguzia kutembea umbali mrefu hadi hospitali za wilaya au mkoa.

Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji kupitia Baraza lake la Madiwani wahakikishe wanasimamia vizuri matumizi ya fedha mbalimbali zinazotolewa na Serikali kwa lengo la kugharamia miradi ya maendeleo.

 Waziri Mkuu amekemea tabia ya baadhi ya wananchi katika maeneo mengi ya mkoa wa Kigoma kudai fidia kwenye maeneo  hata ya mapori na kukwamisha baadhi ya miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa hospitali ya kanda, aliwataka wabadilike.

Awali, alishiriki swala ya Ijumaa katika msikiti wa Mujahidina uliopo eneo la Buzebazeba mijini Kigoma, ambapo alitumia fursa hiyo kuwaasa waumini wa dini ya Kiislam na wananchi kuendelea kulinda amani.

Pia, Waziri Mkuu aliwahamasisha walime zao la michikichi kwani Serikali imeamua kulifufua zao hilo ili waweze kuondokana na umasikini, “wanaotamani kulima michikichi wajiandae wakati utakapofika watasambaziwa miche.”