Majaliwa aagiza Ma RC, DC kufanya operesheni kuondoa rumbesa

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa

Muktasari:

Mbunge wa Mlalo (CCM) Rashid Shangazi ameitaka Serikali ya Tanzania kufanya operesheni nchi nzima ya vifungashio visivyostahiki (lumbesa) ili kuwawezesha wakulima kupata malipo stahiki. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema suala hilo wanalifanyia kazi kwa kutoa maagizo kwa viongozi wa mikoa na wilaya kulisimamia.

Dodoma. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameagiza maofisa ushirika, wakuu wa mikoa (RC) na wilaya (DC) nchini humo kufanya operesheni katika masoko ili kuhakikisha wanunuzi wanafuata utaratibu stahiki wa vifungishio.

Majaliwa ametoa maagizo hayo leo Alhamisi Septemba 12, 2019 bungeni akijibu maswali ya papo kwa hapo wakati akijibu swali la Mbunge wa Mlalo (CCM) Rashid  Shangazi.

Shangazi amesema hivi karibuni  kumekuwa na changamoto ya vifungashio vya rumbesa na visivyo na viwango stahiki.

Amesema cha kusikitisha ni kuwa mamlaka za Serikali zimeshindwa kabisa kudhibiti ufungaji wa mazao kwa mtindo wa rumbesa.

“Je, Serikali iko tayari kuanzisha operesheni maalum nchi nzima kudhibiti tatizo hilo ambalo linawanyong’onyesha wakulima na kuwaletea lindi la umasikini,” amehoji Shangazi.

Akijibu swali, Majaliwa amesema wameanza kuona baadhi ya wanunuzi kutofuata kanuni, taratibu na sheria pindi wanapokwenda kwa wakulima.

Amesema Serikali imeweka utaratibu kwa mazao yote yanayolimwa na kuingia katika masoko yatumie vipimo stahiki ili yaweze kulipa na mkulima aweze kunufaika.

“Lakini muhimu zaidi ni kutumia mizani ambayo haina utata. Lakini imetokea wanunuzi kuwalazimisha wakulima badala ya kipimo sahihi kuongeza nundu ama lumbesa hii haikubaliki.”

“Tumetoa maelekezo sahihi kwa wakuu wa mikoa wote, wakuu wilaya wote, wakurugenzi na maofisa ushirika wanaosimamia masoko wawe wasimamizi pindi mkulima anapouza mazao yake ili vipimo sahihi vinatumika na sio kuongeza nundu,” amesema.